Huyu ndiye Mtanzania wa kwanza kucheza soka Ulaya

HomeMichezo

Huyu ndiye Mtanzania wa kwanza kucheza soka Ulaya

Sunday Manara alizaliwa miaka 67 iliyopita mkoani Kigoma na alianza elimu ya msingi mwaka 1961 katika shule ya White Fathers iliyokuwa Ujiji kabla ya familia yao kuhamia jijini Dar es Salaam.

“Nikiwa shule ya msingi ndiko nilijifunza soka, nilivutiwa na kaka yangu mkubwa ambaye alikuwa mchezaji hivyo nami nikapenda na kuanza kujifunza. Nilianza kama mchezaji wa mtaani katika timu ya Buguruni Stars, kisha nikajiunga na Young Kinya na baadaye timu B ya Yanga iliyokuwa ikiitwa African Boys,” amesema Manara.

Manara anasema, 1969 ndipo alianza rasmi kuichezea Yanga ya wakubwa, baada ya kipaji chake kuonekana na huko alicheza na kaka yake, Kitwana Manara na mdogo wake, Kassim Manara.
Wakati huo alimudu kucheza namba zote za mbele kuanzia namba 7, 8, 9, 10 na 11, na siyo Yanga pekee bali hata timu ya taifa alibadilishwa namba mara kwa mara kutokana na uwezo wake wa kumudu namba zote za mbele.

Maisha ya Ulaya yalivyompa taabu
Mwaka 1976 wakati Yanga inaingia kwenye mgogoro na baadhi ya wachezaji nyota kuondoka kwenye timu hiyo, yeye alitimkia Uholanzi ambako alikwenda kuichezea timu ya Heracles kama mchezaji wa kulipwa.

“Nilipata taabu kidogo na maisha ya Ulaya, kwa mimi mchezaji ambaye nimetoka Dar es Salaam na kwenda Ulaya kwa mara ya kwanza tena kucheza mpira kwa kweli mwanzoni nilisumbuka. Haikuwa rahisi kuzoea mazingira ya soka la Ulaya, aina ya ulaji wa wachezaji na hata tabia zao, siyo siri nilipata taabu hadi kuzoea hali hiyo na mimi kuwa kama wao.”

Alikaa Uholanzi hadi 1978 na kuondoka kwenda kuichezea klabu ya New York Eagles ya Marekani ambayo aliichezea mwaka mmoja na kutimkia Australia kwenye klabu ya Australian mwaka 1980.

“Huko nako nilikaa mwaka mmoja na 1981 nilienda Dubai, Falme za Kiarabu na kujiunga na klabu ya Al-Nasri iliyokuwa miongoni mwa timu kubwa kwenye Ligi Kuu Dubai kabla ya kurejea nyumbani 1984 na kuamua kustaafu,” ameeleza nyota huyo.

Manara apewa jina la kompyuta
“Nilishangaa kusikia naitwa kompyuta, sikujua kitu hicho ni kitu gani, ila ninachokumbuka mimi nilisikia kwa mara ya kwanza mashabiki wakiniita kompyuta mwaka 1975. Jina hilo lilivuma na kuzoeleka, niliamua kuuliza maana ya kompyuta ni nini nikaambiwa ni mashine inayopiga hesabu kwa haraka sana,” amesema Manara.

Licha ya kulikubali jina hilo, lakini hakuwahi kuiona hiyo mashine hadi alipokwenda Ulaya na kuishuhudia kwa macho miaka mitatu baadaye.

Siri yake ya mafanikio

“Mimi nilikuwa nikipenda soka, nakumbuka tulipokuwa wadogo mimi na mdogo wangu Kassim tulikuwa tukiingia chumbani kwetu chini ya uvungu wa kitanda tulikuwa na mipira si chini ya sita.”

Amesimulia kwamba kuna wakati alitoka Ilala akikimbia hadi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kufanya mazoezi ya soka na hakuona taabu kwani alikuwa na mapenzi yaliyopitiliza kwenye soka.

“Nilikuwa na tabia moja, nikiona mchezaji amefanya kitu kizuri uwanjani nikapenda basi mimi nitajifunza hicho kitu ili nimpite, ki-ukweli nilikuwa mtaalamu wa kuiba mbinu za mchezaji mwingine na kuzifanyia kazi.”

Tofauti ya soka zamani na sasa
“Sasa kiongozi ama wa klabu au chama ndiyo anakuwa mmiliki wa mpira, tofauti na zamani kila mmoja alikuwa mmiliki na tulishirikiana kuendeleza soka hapa nchini. Tofauti nyingine, zamani hakukuwa na hujuma ya fedha, lakini sasa mchezaji anataka fedha na kiongozi anataka fedha hivyo kila mmoja kwa nafasi yake anafanya namna yoyote ili apate fedha hata kwa kufanya hujuma,” anasema.

Mechi ya Yanga na Aston Villa ya England
“Ilikuwa ni mechi kubwa na wakati huo Yanga tulikuwa vizuri, nakumbuka ilikuwa ni mwaka 1973, ambapo Aston Villa ndiyo walitangulia kufunga na mimi nikaisawazishia Yanga na kufanya matokeo kuwa 1-1.

Kuhusu Soka la Tanzania
“Nchi nyingine wachezaji wa zamani wanakuwa karibu na benchi la ufundi kwa ajili ya kutoa ushauri, lakini Tanzania kitu hiko hakipo, mchezaji wa zamani hupewi nafasi.
Anasema “Tena ukionekana unachangia unaanza kubezwa, hili ni tatizo, ndiyo sababu kila siku tunazidi kuporomoka badala ya kupanda, mifumo ya soka letu inapotea.”

error: Content is protected !!