Jeshi la Polisi limewaachia mamia ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pamoja na viongozi wao wakuu baada ya kuwakamata ndani ya siku mbili zilizopita kutokana na zuio la kongamano la kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Vijana.
Chadema juzi walieleza kuwa viongozi wao wakuu, Mwenyekiti Taifa, Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti Bara, Tundu Lissu, Katibu Mkuu John Mnyika na viongozi wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) akiwemo Mwenyekiti wao John Pambalu walikamatwa na polisi na wafuasi wengine 469 wakiwemo waliokamatwa wakiwa safarini kuelekea jijini Mbeya.
Kamishna wa Mafunzo na Operesheni wa Polisi, Awadh Haji amewaambia wanahabari usiku wa kuamkia jana jijini Mbeya kuwa walikuwa wamewakamata watu 520 wakiwemo viongozi hao kutokana na kukaidi amri ya polisi ya kutofanya kongamano hilo mkoani Mbeya.
Haji amesema kati ya watu hao waliotiwa nguvuni na polisi, wafuasi 375 wakiwemo wanawake 114 walikamatwa Agosti 11 wakiwemo Lissu na wale waliokuwa safarini kuelekea Mbeya kuhudhuria kongamano hilo walilokuwa wamelipiga marufuku wakidai kuwa limelenga huhatarisha Amani.
“Wote waliokamatwa Morogoro na mikoa mingine wamerejeshwa kwa ‘escort’ (kusindikizwa) ya polisi, wameachiliwa huru na kila mmoja kuendelea na maisha yake lengo lilikuwa ni tusimpe fursa kuja kufanya upuuzi aliotaka kufanya huku Mbeya,” amesema Haji.
Watuhumiwa hao, amesema waliachiwa huru baada ya kufanyiwa mahojiano na jeshi hilo na walibaini walikuwa wanatokea mikoa 11 nchini ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Dodoma, Simiyu na Zanzibar.
Kiongozi huyo wa polisi amesema viongozi wakuu wa Chadema ambao walikamatwa Agosti 11 na 12 nao baada ya mahojiano na taratibu nyingine na wenyewe walirudishwa kwa kusindikizwa na polisi kurudi huko walikotokea na imebainika wengi walitokea Dar es Salaam.
“Lakini kuna viongozi wengine wameachiwa kwa dhamana kwa sababu wana kesi nyingine tofauti na hii waliyofanya,” amesema Haji.
‘Hatutaki ya Kenya’
Licha ya kuwaachia viongozi hao na wafuasi wao, Haji amesema wameimarisha ulinzi mkoani Mbeya kuhakikisha kwamba hawatoi “nafasi kwa wale walioadhamiria vitendo vya uvunjifu wa amani, vurugu na kadhia nyingine kama ambavyo walivyosema wanataka kuigiza yale yaliyofanyika nchi jirani ya Kenya”.
“Hatuwezi kuwapa nafasi wale wahalifu wachache ya kutaka kuchezea na kuharibu amani iliyopo kwa kuiga yale yanayofanyika na nchi jirani,” amesema Haji.
Nchini Kenya mamia ya vijana walijitokeza kufanya maandamano kati ya Juni na Julai mwaka huu kupinga kodi kubwa na ubadhirifu unaofanywa na baadhi ya watumishi wa Serikali ya Rais William Ruto katika matukio yaliyoacha vifo na marejeruhi.
Jeshi la polisi limekosolewa vikali kwa kuwazuia Chadema kufanya kongamano lao ilihali vyama vingine kama Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo wakiruhusiwa kufanya mikutano yao kuadhimisha siku ya kimataifa ya vijana.
Katika utetezi wake, Haji amesema wamekuwa wakishirikiana vizuri na Chadema katika kuimarisha ulinzi kwenye mikutano yao ya hadhara na maandamano lakini safari waliamua kuchukua hatua baada ya baadhi ya viongozi wa Bavicha kutoa matamko yenye viashiria vya kuvunja amani.
“Vyama vingine ambavyo vimefuata taratibu vimefanya hayo maadhimisho kwa sababu hatukubaini kwamba wamepanga kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani,” amesema Haji.
“Unapoona dalili za moshi usisubiri uone moto, ukisubiri moto utokee ina maana unasubiri madhara makubwa.”