Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imebatilisha uteuzi wa Luhaga Mpina kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo, ikisema haukufuata taratibu za chama hicho, hivyo hastahili kuwa mgombea wa nafasi hiyo.
Uamuzi huo, unakuja baada ya ofisi hiyo kuwakutanisha viongozi wa chama hicho na Katibu Mwenezi wa ACT Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala aliyelalamikia kupitishwa kwa Mpina, akidai kulivunja kanuni.
Mpina amekutana na kigingi hicho siku moja kabla ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kufanya uteuzi wa wagombea udiwani, ubunge na urais watakaoshiri Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025.
Baada ya hatua hiyo, inafuata hatua ya kuweka mapingamizi dhidi ya mgombea urais, hatua inayoweza kuwekwa na mgombea mwingine yeyote, msajili wa vyama au Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mwisho wa kuweka pingamizi kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi, ni hadi keshokutwa Agosti 28, saa 10:00 jioni, isipokuwa kama aliyeliweka ni Msajili wa Vyama vya Siasa, ukomo wake ni ndani ya siku 14 baada ya siku ya uteuzi.
Mpina na mgombea mwenza wa urais wake, Fatma Fereji walikwishachukua fomu na INEC za kuomba kuteuliwa kuwania nafasi hiyo na wanatarajia kesho Agosti 27 kuzirejesha kwa ajili ya uteuzi.
Tayari wawili hao wamezunguka mikoani kusaka wadhamini 200 katika kila mkoa kwenye mikoa isiyopungua kumi, ikiwemo miwili ya Zanzibar.