Ofisa Mtendaji, Mgambo wadaiwa kuua mwanafunzi kisa viatu

HomeKitaifa

Ofisa Mtendaji, Mgambo wadaiwa kuua mwanafunzi kisa viatu

Ofisa Mtendaji katika kata moja wilayani Siha mkoani Kilimanjaro na mgambo, wanadaiwa kuwatembezea kipigo wanafunzi wanne na kusababisha kifo cha mmoja wao anayesoma kidato cha pili.

Marehemu ametambulika kwa jina la Bright Arnold (14) na wanafunzi wenzake watatu wa shule ya sekondari Fuka wilayani Siha, wanadaiwa kupigwa ndani ya Ofisi ya Mtendaji huyo wa kata wakituhumiwa kuiba viatu.

Mama MKubwa afunguka

Ruth Munuo ambaye ni mama mkubwa wa marehemu alidai siku ya tukio Juni 17,2022 akiwa anatoka kwenye shughuli zake, alipata taarifa za mwanawe huyo kuchukuliwa na mgambo na kupelekwa Ofisi ya Kata.

“Walimchukua wakidai ameiba raba na alikiri kuzichukua na kuonyesha zilipo, kwa kweli alipigwa kipigo ambacho hakustahili hata kama mtoto alikuwa na makosa,”

Shangazi naye afunguka

Elisifa Mrang’u ambaye ni shangazi wa marehemu, alidai siku hiyo saa 5 asubuhi alielezwa kuwa kuna kijana aliyekuwa ameongozana na mgambo wa kata, walimchukua mwanafunzi huyo na kumpeleka ofisi za kata akidaiwa kuiba viatu.

“Nikiwa sielewi chochote kwenye saa 11:00 jioni nilipita ofisi hizo, nikawaona watu na wanafunzi wanachungulia dirishani na mlangoni, nikauliza kuna nini nikaambiwa kuna wanafunzi wameiba wanapigwa,”

“Nikaambiwa alippoulizwa alikiri na alimtaja mtu aliyekuwa navyo, lakini kaniambia mgambo hao waliendelea kumpiga na kumtaka ataje vitu vingine walivyoiba na watoto wengine wanaoshirikiana huku wakiendelea kumpiga,” alisema Elisifa Marangu, shangazi wa marehemu.

Baada ya kipigo 

Baada ya kumaliza kupigwa na kutoka nje watoto watatu waliweza kusimama, lakini Bright hakuweza kusimama kabisa kwa kuwa alikuwa ameumizwa sana kwenye magoti na kichwani.

Alibebwa na wananchi na kukimbizwa hospitali Kibong’oto kwa pikipiki lakini baadaye hali yake ilizidi kuwa mbaya akahamishwa Hospitali ya KCMC na kesho yake alifariki dunia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alikaririwa akisema Ofisa Mtendaji pamoja na mgambo wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuwapiga watu kadhaa na kusababisha Bright kulazwa KCMC.

 

error: Content is protected !!