Mbinu 7 za kuishi na Boss mkorofi kazini

HomeElimu

Mbinu 7 za kuishi na Boss mkorofi kazini

Katika harakati za kuajiriwa katika kampuni au taasisi fulani inawezekana ikawa umeshawahi kukutana na ‘Boss’ mkorofi na ukashindwa kujua namna ya kukabilina na hali hiyo. Kwa maendeleo binafsi na ya kazi, ni lazima kuwe na mahusiano chanya kazini kati ya mwaajiriwa na msimamizi “Boss”

Wapo ambao huamua kuacha kazi pindi wapitiapo changamoto ya kutokuelewana  Boss lakini kulikimbia tatizo hata siku moja haijawahi kuwa dawa ya tatizo, yakupasa kutafuta suluhu juu ya tatizo hilo, au kutafuta namna iliyo bora ambayo utaweza kuishi na tatizo hilo.

Zifuatazo ni njia za kumkabili ‘Boss’ Mkorofi

1. Tambua tabia ya ‘Boss’ wako
Kutambua tabia ya ‘Boss’ wako kazini ni hatua ya kwanza katika kujifunza namna ya kuishi nae. Tambua ni wakati gani anakuwa na hasira, na pia hasira zake hasa zinatokana na vitu gani. Kuna muda anaweza kuleta hasira za nyumbani kwake kazini, hii mbaya kwa ustawi wa wafanyakazi lakini unapswa kujua hali hii ili umuepueke. Kama, hasira na ukali wa ‘Boss’ ni kutokana na namna mnavyofanya kazi, basi ni lazima mjirekebishe ili kuendana na matakwa yake. Lakini pia kama mfanyakazi, una nafasi ya kuongea na Boss wako ili kumuweka bayana namna ambavyo tabia yake inaweza kuathiri utendaji wako wa kazi (hii inashauriwa isiwe mbele ya watu wenginine).

2. Kuwa makini kwenye uchaguzi wa maneno
Kitu cha msingi zaidi ni kujua unazungumza na nani na kwa wakati gani. Hii haina maana umuogope Boss wako, ila unapaswa umheshimu. Namna nzuri ya kuwasiliana vyema na Boss wako ni kufanya mazungumzo yenu yawe kuhusu kazi, kuelezana changamoto zenu hasa kuhusu kazi na pia kuangalia namna kazi mtaboresha huduma kazini. Kukiwa na mpaka huo basi, itakuwa ni aghalabu sana kuingia kwenye mikwaruzano na Boss wako.

3. Wajibika pale inapobidi
Mikwaruzo na Bosi wako kazini inawezekana ikachochewa na tabia za nyote wawili, (mfanyakazi na Boss wake). Inaweza kuwa rahisi kuzungumzia mapungufu ya Boss wako, lakini ni muhimu zaidi kujambua tabia yako au mwenendo wako kwa Bosi wako, pengine inaweza kuwa chanzo cha mikwaruzo yenu. Kutokuwajibika kurekebisha tabia zako kunaweza kukachochea zaidi vurugu ofisi kwako.

4. Usipende kuzungumza mapungufu ya Boss wako
Epuka sana kuzungumzia mapungufu ya Boss wako kwa wafanyakazi wenzako, kwani hii inaweza kuchochea vurugu zaidi kazini. Kile ambacho unapitia na Boss wako sio lazima kila mfanyakazi akipitie au akifahamu, hivyo haina ulazima sana kuzungumza na kila mtu kazini kueleza kadhia yako. Unaweza kuomba ushauri, lakini uwe makini kwa sababu unaweza kubadili mawazo ya wafanyakazi wenzako juu ya Boss wao na pengine kupelekea Boss wako kutazamwa zaidi katika taswira ambayo wewe unaiwasilisha kwao kila mara.

                         > Mbinu 5 za kumaliza tatizo la uvivu kazini

5. Jiongeze kutambua matokeo, matarajio na matarajio
Chukua muda kutambua Boss wako anatarajia kitu gani kutoka kwako na malengo yake ni yapi. Hii itakufanya muda wote uwe mbele ya wakati, utakuwa una uwezo wa kufanya kazi bila kuhimizwa. Fanya kile ambacho Boss wako anataka ufanye, kama anahitaji umpatie ripoti fulani kwa muda fulani, basi fanya hivyo sio mpaka ukumbushwe. Kutambua Bosi wako anataka nini na ukafanya kwa usahihi, inaonesha heshima na namna gani unajali kazi yako.

6. Jifunze stadi za uongozi
Katika nyakati zote ngumu kazini unazopitia na Boss wako, usizichukulie tu kama nyakati mbaya, bali chukulia kama Chuo au Shule ya kujifunza uongozi. Kupitia Bosi wako hata wewe mwenyewe, ni wakati ambao utaweza kujua ni namna gani utaweza kuishi na watu wenye tabia tofauti, na namna ya kuwasilisha mawazo yako kwao.

7. Tambua aina ya mawasiliano ya Bosi wako
Kuna namna nyingi za kuwasiliana, kuna watu hupendelea barua pepe, wengine hupendelea kufuatwa na wengine hupenda kupigiwa simu. Mtindo wa mawasiliano unaopaswa kuutumia ni ule anaopenda kuutumia Boss wako, sio unaopenda wewe. Kama Boss wako anapenda Barua pepe, basi wasiliana nae kwa njia hiyo. Kama ni kupiga simu, jua ni muda gani hupokea simu na muda gani usimpigie simu. Kutambua haya ni muhimu sana kwani kutaboresha uhusiano wako kazini.

Zipo faida nyingi zinazotokana na kufahamu kuishi na Boss Mkorofi, kama kupunguza msongo, kuboresha mahusiano kazini na kuongoza uzalishaji na ufanisi kazini.

error: Content is protected !!