Baada ya kifo cha panya Magawa hatimaye mrithi wake amepatikana anafahamika kwa jina la Renin ambapo taarifa zinasema tayari yupo nchini Cambodia kuendeleza majukumu yake.
Pendo Msegu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo(SUA), mkufunzi wa panya hao kwenye mradi wa Apopo alisema kuwa Renin ameonekana kuwa na sifa za utendaji wa kazi wa kiwango cha juu na hufanya kazi hiyo kwa muda mfupi, akilinganishwa na wenzake.
“Mrithi wa Magawa ni Renin na huyu panya yupo nchini Cambodia kuendelea na majukumu ya kazi anayofanya na wenzake huko, lakini hata kazi anazopewa amekuwa akizifanya kwa ufanisi na kwa ufanisi na kwa muda mfupi,” alisema.
Mkufunzi huyo alieleza kuwa Renin anafuata nyayi za Magawa za kutokuwa na mwenza ili kutekeleza majukumu yake ya kunusa mabomu yaliyotegwa ardhini na pia kuongeza kuwa hadi kifo chake, Magawa liyezaliwa Novemba 5 mwaka 2014, alinusa na kubaini mabomu zaidi ya 100 yaliyotegwa ardhini.