Mafanikio ya ziara ya Waziri January Makamba Uarabuni

HomeKitaifa

Mafanikio ya ziara ya Waziri January Makamba Uarabuni

Wizara ya  Nishati imetoa taarifa kuhusu ziara iliyofanywa na Waziri January Makamba kuanzia tarehe 22 hadi 29 Oktoba 2021 katika nchi tatu (Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Algeria) zinazozalisha mafuta kwa wingi na kuuza duniani kote.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa leo, pamoja na mambo mengine ziara hiyo ililenga kuzungumza na nchi hizo ili kuangalia uwezekano wa Serikali, kupitia Shirika la Mafuta Tanzania (TPDC), kununua mafuta moja kwa moja kwenye mitambo yao ya kuzalisha mafuta na hivyo kupunguza gharama zinazowekwa na wanunuzi wa kati.

Pia ziara hiyo ilikuwa na madhumuni ya Tanzania kubadilishana uzoefu na nchi hizo kuhusu uendeshaji wa sekta ya mafuta na gesi na kuimarisha mahusiano yaliyopo na kujenga ushirikiano mpya katika eneo la mafuta ili Tanzania ipate jawabu la kudumu la kujihakikishia upatikanaji wa uhakika wa mafuta na kwa bei isiyopanda ghafla na kwa kiwango kikubwa.

Katika taarifa hiyo Waziri January Makamba amesema “nilifanikiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Mawaziri wenzangu wa Nishati, viongozi wengine waandamizi na wakuu wa mashirika ya mafuta ya taifa ya nchi hizo. Kutokana na heshima ya nchi yetu na Rais wetu, na urafiki wa nchi yetu na nchi hizi, nilipokelewa vizuri na viongozi wote katika nchi zote hizi na walipokea na kukubali hoja na haja ya mashirikiano katika sekta hii ya mafuta. Kwa kifupi, yale yote ambayo nchi yetu iliyapendekeza kwenye nchi hizi yamekubalika.”

Ameanisha mafanikio yaliyopatikana katika ziara hiyo ambayo ni pamoja na Tanzania kukubaliana na mataifa hayo matatu kushirikiana katika masuala ya mafuta na gesi ambapo baada ya taratibu za kiserikali na kisheria kukamilika, makubaliano hayo  yatatangazwa.

Pia imeelezwa kwamba kwa mara ya kwanza, azma ya miaka mingi ya Serikali, kununua shehena ya mafuta moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji sasa imetimia.

Waziri Makamba ameleza “Hata kabla ya mwisho wa safari yetu, mnamo tarehe 28 Oktoba 2021, tuliiwezesha TPDC kushiriki zabuni ya kiushindani na makampuni mengine ya kimataifa ambayo kila mwezi hushiriki zabuni ya kuleta mafuta nchini. TPDC imefanikiwa kushinda sehemu kubwa ya zabuni hiyo kwa kutoa bei ndogo zaidi ya kuagiza mafuta ya dizeli nchini kwa mwezi wa Disemba mwaka huu. Hali hii itapunguza makali ya bei ya mafuta ya dizeli kwa mwezi Disemba.”

Mafanikio mengine ni Wizara ya Nishati kuweza kushawishi nchi tatu zilizotembelewa  kushirikiana na Tanzania kujenga kituo kikubwa cha upokeaji na uhifadhi mkubwa wa mafuta (fuel terminal) kwa ajili ya soko la ndani ya Tanzania lakini kwa mahitaji ya nchi za Afrika Mashariki na Kati na nyingine za mbali pale itakapohitajika. Makamba ameeleza kwamba kituo hicho kitaihakikishia Tanzania kuwa na kiasi cha kutosha cha mafuta ndani ya nchi wakati wote.

Aidha Waziri Makamba ameeleza kwamba daada ya wiki mbili kuanzia sasa, kutakuwa na ziara za viongozi na watalaam kutoka katika nchi walizotembelea kuja Tanzania kwa ajili ya kukamilisha taratibu za utekelezaji wa makubaliano yetu kwenye maeneo waliyokubaliana kushirikiana.

Katika kuhitimisha taarifa hiyo, Waziri January Makamba ameeleza kuwa, bei ya mafuta nchini kwa kiasi kikubwa inachangiwa na bei za mafuta duniani, ambazo Serikali ina nafasi ndogo kwenye kuzidhibiti. Amesema, hata hivyo Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali, kuhakikisha kwamba yale yaliyo ndani ya uwezo wa Serikali ya Tanzania katika kudhibiti bei ya mafuta yanayafanyiwa kazi.

 

error: Content is protected !!