Wakati dunia ikiendelea na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, nguvu kubwa ielekezwe kuwalinda wasichana ambao wamekuwa wahanga wa ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa ripoti ya masuala ya Ukimwi duniani ya mwaka 2022 inayotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Ukimwi Duniani (UNAIDS), wanawake na wasichana wapo hatarini kupata maambukizi ya VVU kuliko wenzao wa kiume.
“Kila dakika tatu (wasichana) wana uwezekano wa kupata VVU mara tatu zaidi ya vijana wa kiume wa rika moja Kusini mwa Jangwa la Sahara,” imesema ripoti hiyo.
Ripoti hiyo imeshauri wadau wa masuala ya afya kuongeza kasi ya kuwafikia wasichana kwa elimu sahihi ya masuala ya uzazi na namna wanavyoweza kujikinga wasipate ugonjwa huo.
Hatua hiyo itasaidia wasichana kutimiza ndoto zao ikiwemo kujikwamua kiuchumi na kielimu.