Serikali ya Tanzania imesema ya kwamba miradi yote mikubwa inayotekelezwa nchini humo inafuata sheria na kanuni za kimataifa ikiwemo za utunzaji wa mazingira na kuheshimu haki za binadamu huku ikifanya miradi yake kwa manufaa ya wananchi wake.
Waziri wa Nishati, Januari Makamba ametoa kauli hiyo Ijumaa Septemba 16, 2022 ikiwa ni sehemu ya ufafanuzi ya maazimio yaliyotolewa siku tatu na Bunge la Ulaya (EU) kuhusu utekelezaji wa mradi huo.
Waziri wa Nishati nchini Tanzania, Januari Makamba amesema hakutakuwa na athari zozote za kimazingira wakati wa utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha Mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima Uganda hadi Chongoleani Tanga kwani tahadhari zote zilizingatiwa kitalaamu.
Makamba amesema Tanzania inazingatia vigezo vya kimataifa katika miradi yake ikiwemo ule wa bomba la mafuta kutoka Uganda mpaka Tanga nchini Tanza na kwamba hakuna kinachokiukwa kama azimio la bunge hilo linavyoeleza.
Makamba amesema, “Nimefuatilia mapendekezo na Azimio la Bunge la Umoja wa Ulaya kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu na uharibifu wa mazingira, Nimeona wameshauri juu ya mradi na athari zake. Serikali ya Tanzania imefuata taratibu zote za kuhakikisha haki za watu na mazingira zinalindwa lakini hakuna kilichokiukwa…
“Tumelipa fidia wananchi wote ambao maeneo yao yapo kwenye eneo la mradi, hakuna yoyote aliyelazimishwa au kukamatwa kwa nguvu. Lakini pia tumefuata kanuni zote zinazohusu mazingira ili mradi huu usidhuru mazingira.
“Kilichopo ni kuwa Tanzania ina kila haki ya kuhakikisha wananchi wake wananufaika na rasilimali zilizopo kama ilivyo kwa nchi zilizoendelea ambazo wananchi wake wananufaika na miradi hiyo”, amesema Waziri Makamba.
Wakati huo huo, Bunge la Uganda limelaani azimio la bunge la Umoja wa Ulaya linalozitaka Uganda na Tanzania kusitisha maendeleo ya miradi yao ya mafuta na gesi katika ukanda wa Afrika Mashariki.