Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema Jeshi hilo limepiga marufuku kwa mtu asiyehusika kufika chini ya Daraja hilo kutokana na sababu za kiusalama.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kamanda Muliro alisema Jeshi hilo linawashikilia watu 12 kwa mahojiano ambapo wawili kati yao walikutwa wakijaribu kufungua baadhi ya vyuma ambavyo vinatumika kama ngazi na kutaka kuchukua vyuma hivyo kwa shughuli binafsi.
“Tunataka kujua wanachukua kwa ajili ya nini na wanavipeleka kwa nani? Uchunguzi unaendelea na ukikamilika watafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo,” alibainisha.
Aidha, Kamanda Muliro alisema daraja hilo limekuwa likilindwa kwani thamani yake ni kubwa hivyo jeshi halitakubaliana wala kuruhusu mtu yeyote au kikundi cha watu kufanya hujuma kwenye daraja hilo.
“Daraja hili halina vyuma chakavu, ni marufuku kwa mtu ambaye hahusiki na masuala ya kiufundi ya ujenzi au usimamizi wa daraja hili kuwa hapo, tukimkuta tutamkamata na kumhoji kwa kina madhumuni yake ni nini,” alisema Kamanda Muliro.