Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na watu wenye ulemavu , Patrobas Katambi amesema mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zinatarajiwa kuzinduliwa mkoani Njombe zikilenga kumulika uovu na ufisadi kwenye miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini.
Mbio hizo zitazinduliwa na Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango huku hatua zikiwa zimechukuliwa kwenye miradi ambayo iligundulika kuwa na dosari katika mbio hizo mwaka 2021.
Miradi ambayo ilikidhi vigezo ilizinduliwa na isiyokidhi vigezo ilikataliwa ili uchunguzi zaidi ufanyike na hatua zichukuliwe, Akizungumzia miradi iliyokataliwa aliitaja kuwa ni miradi 49 yenye thamani ya Sh. bilioni 65.3 ambapo Rais Samia aliagiza uchunguzi ufanyike na hatua stahiki zichukuliwe.
“Kuna wakurugenzi waliopoteza nafasi zao, kuna watumishi ambao ni wataalamu walipoteza nafasi zao, kuna wengine kesi zao bado zinaendelea, sasa jambo linapokuwa mahakamani hupaswi kulizungumzia kwa kuwa ndicho chombo pekee cha uamuzi wa haki”
“Ukifatilia vizuri utabaini kuna baadhi ya halmashauri kuna kesi za PCCB (TAKUKURU) ambazo zipo hatua mbalimbali, pia siku ya uzinduzi wa mwenge itatolewa tathmini Mwenge uliopita na huu unaofata na mambo ya kuzingatia, ambapo Mheshimiwa Makamu wa Rais kuna mambo atayasema ambayo yatakuwa ni mrejesho wa kile kilichofanyika kwa mwaka uliopita. Kwahiyo sitaki kumuingilia Makamu wa Rais katika hilo”. alifafanua Katambi.
Aidha mbio za mwenge wa Uhuru mwaka huu zinatarajiwa kufika kwenye mikoa 31 na halmashauri 195, zikibeba ujumbe mkuu wa kuhamasisha sensa ya watu na makazi.
Katambi anasema mwenge ni jicho la Rais pamoja na kwamba kuna vyombo vingine lakini vijana wanaokimbiza mwenge huo huwa na utaalamu wa ukaguzi wa miradi.