Nunua luku mapema

HomeKitaifa

Nunua luku mapema

Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema huduma ya kununua umeme kupitia Luku itakosekana kwa muda wa masaa mawili usiku kuamkia Alhamisi Juni 9 mwaka huu ili kupisha matengenezo ya mifumo yake.

Tanesco imetoa taarifa hiyo kupitia Meneja Mwandamizi wa Tehama Cliff Maregeli alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Juni 6 makao makuu ya Tanesco Jijini Dar es Salaam

‘Tunategemea kwamba kwa muda wa masaa mawili kuanzia saa sita usiku mpaka saa saba hivi, wateja hawataweza kununua umeme wakati tukiwa tunafanya matengenezo,” amesema Maregeli.

Tanesco imewataka wateja wake kununua umeme wa ziada ili kuepuka usumbufu wowote utakaoweza kujitokeza au hata kama ikitokea hitilafu yoyote waweze kustahimili  wakati wanafanya matengenezo.

Matengenezo hayo yatafanyika kati mifumo ya kuuza umeme kwa ulipaji wa kabla yaani Luku, katika kituo cha kujikinga na majanga. 

Pia yataliweka shirika katika hali nzuri ya kuhimili hitilafu yoyote itakayoweza kujitokeza kwenye mfumo wa manunuzi. 

Sambamba na hilo matengenezo hayo yataongeza utayari wa kuwahudumia wateja pale itakapotokea hitilafu katika mfumo mkuu kwa sababu watakuwa na seti mbili za mifumo zitakazowawezesha wateja kupata huduma endelevu.

error: Content is protected !!