RAIS wa Kenya, William Ruto amemteua Profesa, Kithure Kindiki kuwa naibu rais akichukuwa nafasi ya Rigathi Gachagua, ambaye aliondolewa madarakani na maseneta jana.
Prof. Kindiki ambaye anahudumu kama Waziri wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa, atahitaji idhini ya bunge kabla ya kushika nafasi ya rasmi nafasi hiyo.
Aidha, Bunge lazima lipigie kura uteuzi huo ndani ya siku 60, baada ya kupokea jina hilo. Baada ya kuidhinishwa, mteule huyo atateuliwa rasmi na Rais kuwa naibu wake.
Prof. Kindiki alizaliwa miaka 52 iliyopita katika kijiji cha Irunduni, Kaunti ya Tharaka Nithi. Kindiki alisoma Shule ya Msingi ya Irunduni, kisha Shule ya Lenana, kabla ya kupata shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.
Baadaye alipata Shahada ya Uzamili na Uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Pretoria. Aliporejea katika taaluma, alifundisha sheria katika vyuo vikuu vya Moi na Nairobi na aliwahi kuwa mhadhiri nje ya nchi.
Kindiki aliingia katika utumishi wa umma 2008 alipoteuliwa kuwa Katibu wa Uwiano wa Kitaifa na Maridhiano na marehemu Rais Mwai Kibaki. Alijiuzulu baada ya miezi mitatu, akitaja ukosefu wa nia ya kisiasa ya kuwapa makazi waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.
Alipata umaarufu baada ya Ruto kumteua katika timu yake ya wanasheria wakati wa kesi ya uhalifu dhidi ya ubinadamu katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Kindiki aliingia kwenye siasa na kuwania kiti cha Seneti cha Tharaka Nithi mnamo 2013 chini ya chama cha TNA.
Alichaguliwa kuhudumu mihula miwili, akipanda wadhifa wa Naibu Spika wakati wa muhula wake wa pili. Hata hivyo, mvutano ulipozidi kukua kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais Ruto, Kindiki alikabiliwa na changamoto katika Seneti na kuenguliwa.
Tangu wakati huo amehudumu kama Waziri wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa katika Baraza la Mawaziri la kwanza na lililoundwa upya la Rais Ruto.