Rais Samia aagiza kuanzishwa kwa tovuti za kumbukumbu za viongozi

HomeKitaifa

Rais Samia aagiza kuanzishwa kwa tovuti za kumbukumbu za viongozi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameagiza kuanzishwa kwa tovuti ya Serikali ya kuhifadhi kumbukumbu za viongozi waliowahi kuhudumu katika nyadhifa mbalimbali wakiwemo marais wastaafu pamoja na mawaziri wakuu.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika hafla ya wa tovuti ya nyaraka za aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na Katibu Mkuu wa Umoja wa Afrika (AU) Dk. Salim Ahmed Salim, leo Septemba 30, 2023 amewaambia washiriki kuwa tovuti hiyo itasaidia kutambua michango ya viongozi, historia ya nchi na Bara la Afrika.

“Tovuti kama hizi zinasaidia kukuza na kuimarisha uelewa wa juhudi za kila mmoja wetu, historia ya nchi yetu na Bara la Afrika, shughuli hii imefungua macho umuhimu wa kufungua tovuti hizi…

…twende kwenye muelekeo huu kama wa Dk. Salim tukatengeneze tovuti ya Serikali ya kuweka kumbukumbu za viongozi wetu,” amesema Rais Samia jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Rais Samia tovuti ya Dk. Salim inaakisi safari ya maisha yake kama kiongozi, mwanasiasa na mwanadiplomasia mahiri, huku ikitoa nafasi kwa watu kufahamu historia yake,Taifa lake na Bara la Afrika.

“Binafsi nimepitia tovuti hii na nimebaini kwa mara ya kwanza kutakuwa na tovuti ya kipekee inayoakisi historia ya nchi yetu kupitia darubini na simulizi za Dk. Salim Ahmed Salim,” ameongeza Rais Samia.

Tovuti hiyo ni muunganiko wa hotuba, barua, makala zilizokatwa kutoka magazetini, machapisho ya kitafiti, picha pamoja na video kumhusu Dk. Salim ambavyo vinaleta shauku na chachu ya kujifunza kutoka kwake.

Hata hivyo, uwepo wa tovuti ya rasmi ya Serikali huenda ukaleta ahueni kwa kurahisisha upatikanaji wa tawasifu na historia za viongozi wa Taifa kwa kuwa kwa muda mrefu hakukuwa na utaratibu maalumu wa kuhifadhi kumbukumbu hizo.

Baadhi ya viongozi wachache hutumia njia ya vitabu kuwasilisha historia na kumbukumbu zao ambapo wakiwemo marais wastaafu wa Tanzania, Hayati Benjamin Mkapa, na Ali Hassan Mwinyi huku Rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Mrisho Kikwete akiwa mbioni kuandika kitabu chake.

error: Content is protected !!