Rais Samia aeleza umuhimu wa sekta binafsi

HomeKitaifa

Rais Samia aeleza umuhimu wa sekta binafsi

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amesema kuna umuhimu kwa viongozi na watendaji wa Serikali kutathimini utekelezaji wa mkakati wa ushirikiano kati ya Serikali na Sekta binafsi ili kuhakikisha lengo la kuwapatia huduma bora za afya wananchi wote linafikiwa.

Mheshimiwa Samia amesema hayo Julai 14, 2022 katika Kongamano la Pili la Kumbukizi ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu , Hayati William Benjamin Mkapa lililofanyika Hoteli ya Golden Tulip Airport Zanzibar.

Amesema ni mwaka mmoja sasa tangu uzinduzi wa mkakati huo kufanyika, hivyo kuna umuhimu kwa viongozi na watendaji serikalini kutathimini wapi azma hiyo imefikia, akibainisha haja ya kujiuliza utekelezaji wa mkakati huo, iwapo maneno yanaendana na matendo.

Amesema kumekuwa na taarifa mara kadhaa kuwa watendaji hao wa Serikali hufuatwa na watendaji kutoka sekta binafsi, lakini matokeo yake ni kuwazungusha hadi kufikia hatua ya kukata tamaa.

“Je? Yale tunayoyasema midomoni ya kufanyakazi na sekta binafsi, lini tutayatekeleza, baadhi yetu bado tumeelemewa na kasumba,”amesema.

Hata hivyo, Rais Samia ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na sekta binafsi katika hatua ya kuhakikisha huduma bora za afya zinawafikia wananchi wote.

Akigusia Kauli mbiu ya Kongamano hilo isemayo “Ushupavu na Uongozi, chachu ya mabadiliko”,Rais Samia amesema, Watanzania hawana budi kuishirikisha kikamilifu sekta binafsi endapo wanahitaji kwenda kwa kasi na kufikia lengo la Afya Bora kwa wote ifikapo mwaka 2030.

Alieleza kuwa, bado dhana ya kuwa sekta binafsi ni mshirika muhimu katika maendeleo haijaaminika na kusema kuwa Dunia ya sasa ni ya uchumi wa soko inayoendeshwa kwa ubia, hivyo Serikali itashirikiana na sekta binafsi ili kufikia lengo la kutoa huduma bora za afya kwa wananchi wote.

Aidha, aliwataka watendaji kutoka sekta binafsi kuzingatia kuwa Afya ni huduma na sio biashara.

error: Content is protected !!