Maana ya ujio wa Kamala nchini

HomeKitaifa

Maana ya ujio wa Kamala nchini

Kwa mara ya kwanza, Kamala Harris, Makamu wa Rais wa Marekani atakanyaga ardhi ya Tanzania kesho Machi 29.

Safari yake ina umuhimu mkubwa kwa Tanzania kwa sababu ni miongoni mwa nchi tatu zilizochaguliwa na Marekani kutembelewa na kiongozi wake wa ngazi ya juu.

Nchi nyingine ni Ghana na Zambia.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ikulu ya Marekani Machi 24, 2023, Kamala anatarajia kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kesho mchana akitokea Accra, Ghana katika ziara ya siku mbili.

Atakayofanya akiwa Tanzania

Kamala ambaye ni Makamu wa Rais mwanamke wa kwanza wa Marekani, atakapowasili nchini kesho atapokelewa na mwenyeji wake na kuendelea na shughuli mbalimbali.

Alhamis Machi 30 atakutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Samia Suluhu Hassan ambapo huenda watakayozungumza yatajikita zaidi katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi wa nchi hizo mbili.

Siku hiyo hiyo, atashiriki hafla na kuweka shada la maua ikiwa ni kumbukizi ya shambulio la bomu linalodaiwa kutekelezwa na kundi lenye msimamo mkali la Jihad katika Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania mwaka 1998.

Shambulio hilo la bomu ambalo pia lilitekelezwa katika Ubalozi wa Marekani nchini Kenya liliangamiza maisha ya watu takriban 244 na kuwaacha wengine majeruhi na ulemavu.

Kukamilika kwa ratiba hiyo kutamuwezesha kukutana na wajasiriamali vijana katika moja ya kituo atamizi kilichopo jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iliyotolewa wiki mbili zilizopita, Kamala ambaye ni Mmarekani mweusi pia atatembelea Makumbusho ya Taifa ya Tanzania (NMT).

Alhamis ndiyo itakuwa siku ya mwisho ya ziara ya kihistoria ya kiongozi huyo nchini ambapo siku inayofuata ya Ijumaa ataelekea Zambia kukamilisha ziara yake ya Afrika.

Akiwa nchini humo atakutana na kufanya mazungumzo na Rais Hakainde Hichilema. Pia atatumia siku yake katika kujadili namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ustahimilivu na usalama wa chakula.

“Tunatarajia atakutana na wawekezaji wa sekta ya umma na binafsi barani kote (Afrika) na atashirikiana na wale wanaohusika katika juhudi hizi za kustahimili hali ya hewa na usalama wa chakula,” imeeleza taarifa ya Ikulu ya Marekani.

Jumamosi, Aprili 1, Makamu wa Rais atakutana na viongozi wa kibiashara na wahisani wa Afrika na Marekani, ili kujadili ushirikishwaji wa kidijitali na kifedha katika bara hilo. Watajadili jinsi ya kushirikiana vyema pamoja na kuendeleza kazi ya safari yake na ahadi zote ambazo atazitoa kwenye safari yake.

“Na ataondoka Lusaka Jumamosi jioni na kurejea Washington Jumapili asubuhi,” imeeleza taarifa hiyo.

Kwa nini anakuja Tanzania?

Aprili 15, 2022, Rais Samia na Kamala walikutana katika Ikulu ya Marekani mjini Washington na kuahidi kuimarisha uhusiano wa mataifa hayo mawili.

Ziara ya Makamu wa Rais nchini Tanzania itaendeleza juhudi za kupanua upatikanaji wa uchumi wa kidijitali, kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na ustahimilivu, na kuimarisha uhusiano wa kibiashara na uwekezaji, ikijumuisha uvumbuzi, ujasiriamali na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi.Sekta nyingine zitakazoguswa ni pamoja na afya, kilimo, utalii, uchukuzi, uchumi wa bluu na mawasiliano.

Ziara hiyo ni utekelezaji wa kauli aliyoitoa Kamala katika mkutano wa viongozi wa Afrika na Marekani Desemba 2022 ambapo aliweka wazi kuwa ubunifu na mawazo ya Kiafrika yatatengeneza mustakabali wa dunia.

Pia alisema Marekani imejitolea kuwekeza katika ustadi na ubunifu ambao umeenea katika bara zima ili kufungua milango ya ukuaji wa uchumi na fursa mbalimbali.

error: Content is protected !!