Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameahidi kwenda kutekeleza kikamilifu mawazo yote yaliyoanzishwa na mtanguluzi wake Rais wa awamu ya tano, Hayati Dk. John Pombe Magufuli huku akitaja kuwa moja ya maono yake ni kukamilisha miundombinu yote iliyoanzishwa.
“Kwa bahati nzuri muundaji wa suala hili aliyetekeleza maono ya baba wa taifa kuhamia Dodoma, akataka kuipanga Dodoma kwa bahati Mungu amemchukua mapema lakini aliniachia urithi mzito nami niliahidi mawazo yote aliyoyaanzisha nakwenda kuyatekeleza kikamilifu,” alisema Rais Samia Suluhu.
Amezungumza hayo wakati wa uwekaji wa jiwe barabara ya mzunguko wa nje ya jiji la Dodoma huku akiongezea kwa kusema kwamba baada ya mradi huo kukamilika utakuza uzalishaji na usafirishaji.
“Mradi huu utakapo kamilika utakuwa ni kichocheo muhimu cha kukuza uzalishaji na usafirishaji, kwa sababu uzalishaji unakua kwenye soko, barabara hii inakwenda kutupeleka kwenye masoko ya mazao yetu ya kilimo lakini pia bidhaa za viwandani, barabara hii inakwenda kutufungulia masoko ili Tanzania tuweze kuzalisha zaidi na zaidi,” alisema Rais Samia Suluhu.