Rais Samia amuunga mkono Raila Odinga AU

HomeKimataifa

Rais Samia amuunga mkono Raila Odinga AU

Nairobi, Kenya – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amempongeza kwa dhati Mheshimiwa Raila Amolo Odinga kwa uongozi wake wa Kipan-African na uwezo wake wa kuchochea maendeleo barani Afrika. Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kampeni za Mheshimiwa Odinga kwa nafasi ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), Rais Samia alieleza kuwa Tanzania inamuunga mkono rasmi kiongozi huyo wa Kenya kutokana na imani yake thabiti katika muungano wa Afrika na uwezo wa kuleta mabadiliko ya vitendo.

Rais Samia alisisitiza kuwa, licha ya mafanikio yaliyopatikana na Umoja wa Afrika katika kutekeleza ajenda ya 263, kuna haja ya kuimarisha umoja ndani ya AU. Alibainisha kwamba kukamilisha mageuzi ya taasisi za Umoja huo na kuimarisha uwajibikaji ni hatua muhimu katika kuhakikisha malengo ya Afrika yanafikiwa. Pia aliongeza kuwa ni lazima AU ipate uwezo wa “kuzima bunduki” barani Afrika na kuweka msingi wa amani na utulivu kwa ajili ya maendeleo ya muda mrefu.

“Umoja wa Afrika unahitaji kuongoza ajenda ya maendeleo kwa kuhakikisha utekelezaji wa mipango ya miundombinu na kuimarisha muunganisho wa bara letu,” alisema Rais Samia. Aliongeza kuwa sauti ya Afrika inapaswa kusikika kwa uwazi kwenye majadiliano ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, nishati, biashara ya haki, na maendeleo ya sheria za kimataifa.

Katika hotuba yake, Rais Samia alieleza kuwa Tanzania inamtambua Odinga kama anayeheshimika na viongozi wengi wa Afrika. Alimuelezea kama kiongozi mwenye hekima na uwezo wa kufanikisha utekelezaji wa ajenda muhimu kwa maendeleo ya Afrika.

Kwa kumalizia, Rais Samia alisema, “Baba anatosha,” akisisitiza kwamba Raila Odinga ana sifa zote za kuwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) na kuendeleza ndoto za waasisi wa bara hili kwa maendeleo, heshima, na umoja wa Afrika.

error: Content is protected !!