Rais Samia Suluhu Hassan ameungana na viongozi mbalimbali kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais mteule wa Nigeria, Bola Tinubu, aliyeapishwa jana Mei 29, 2023 kufuatia kuibuka mshindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika Februali 25, 2023.
Sherehe hizo zimefanyika katika viwanja vya ‘The Eagle Square’ nchini Nigeria ambapo viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Rais wa Rwanda Paul Kagame na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa.
Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune, Katibu mkuu wa Baraza la Mawaziri nchini Kenya Musalia Mudavadi, ambaye amemuwakilisha Rais wa nchi hiyo William Ruto pamoja na wajumbe kutoka nchi za Marekani , Uingereza na China ni baadhi ya viongozi wengine waliofika katika sherehe hiyo.
Rais Bola Tinubu aliyeapishwa leo mbele ya umati wa wananchi wa Nigeria anakuwa Rais wa 16 kushika madaraka hayo tangu nchi hiyo ipate uhuru mwaka 1960.
Tinubu mwenye umri wa miaka 71 alishinda kiti hicho kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 25 Februari 2023 ambapo kwa mujibu wa tovuti ya ‘Premium Times’ ya nchini Nigeria Rais huyo alipata kura milioni 8.7 na kuwashinda wagombea wengine 17.
Sherehe hizo pia zilihusiha kuapishwa kwa Makamu wa Rais mteule Kashim Shetima aliyeapa mbele ya jaji mkuu wa nchi hiyo Olukayode Ariwoola.
Mahusiano ya Tanzania na Nigeria
Ushiriki wa Rais Samia katika sherehe hizo ni mwendelezo wa mahusiano baina ya mataifa haya mawili ambayo yamekuwa yakishirikiana katika nyanja mbalimbali ikiwemo biashara yaliyoimarika zaidi mwaka 2022.
Kwa mujibu wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya nje Liberata Mulamula biashara kati ya nchi hizo imeongezeka kutoka Sh23 bilioni mwaka 2020 hadi Sh24 bilioni mwaka 2021.
Kama matunda ya ushirikiano huo ulioasisiwa mwaka 1962, Tanzania inanufaika na uwekezaji uliofanywa na raia wa Nigeria nchini akiwemo Aliko Dangote ambaye anazalisha saruji kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.