Rais Samia Suluhu ameteuliwa rasmi kuwa Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Kituo cha Dunia cha Uhimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi (Advisory Board of the Global Centre on Adaptaion- GCA).
Taarifa hiyo ilitolewa na Mhe. Ban Ki- moo, mwenyekiti wa Bodi ya GCA na Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa alipokutana na Mhe. Rais pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi uliofanyika Nairobi, Kenya.
Heshima ya utambuzi huo ni kutokana na uongozi mahiri wa Rais Samia Suluhu katika jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi Afrika na duniani kote ambapo Tanzania ni kinara kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali barani Afrika.
GCA ni taasisi kubwa duniani inayosimamia masuala ya uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi, ambapo hadi sasa imeweza kufanikisha upatikanaji zaidi ya dola za Marekani bilioni 50. Tanzania ni miongoni mwa nchi za kwanza zitakazonufaika na fedha hizo katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.