Rais Samia awahimiza Watanzania kujenga tamaduni za kupima afya mara kwa mara

HomeKitaifa

Rais Samia awahimiza Watanzania kujenga tamaduni za kupima afya mara kwa mara

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewahimiza Watanzania kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara ili kugundua magonjwa ya saratani mapema, akisisitiza kuwa saratani si hukumu ya kifo endapo itagundulika mapema na mgonjwa kupata matibabu sahihi.

Rais Samia ametoa wito huo leo wakati akifungua rasmi Jengo la Tiba ya Mionzi kwa Wagonjwa wa Saratani katika Hospitali ya Kanda ya KCMC, mkoani Kilimanjaro, akibainisha kuwa serikali imeendelea kuboresha huduma za afya ili kuhakikisha wagonjwa wanapata tiba karibu na maeneo yao.

Akizungumza na wananchi pamoja na viongozi wa dini waliohudhuria hafla hiyo, Rais Samia alisema ni muhimu jamii kuondokana na hofu na dhana potofu kuhusu saratani, na badala yake kujenga utamaduni wa uchunguzi wa mapema.

“Naungana na viongozi wa dini kusisitiza kuwa saratani si hukumu ya kifo. Ukipima mapema na kufuata ushauri wa wataalamu, nafasi ya kupona inaongezeka kwa kiasi kikubwa,” alisema Rais Samia.

Alisisitiza zaidi kwa wanaume kutoogopa wala kuona aibu kupima afya ya tezi dume, akieleza kuwa mara nyingi wagonjwa huchelewa hospitalini hali inayofanya matibabu kuwa magumu.

“Wanaume wasione aibu. Kupima mapema ni muhimu. Ukisubiri hadi maumivu yaongezeke au ugonjwa ushaendelea, unakuwa umechelewa,” aliongeza.

Kwa upande wa wanawake, Rais Samia aliwahimiza kufanya uchunguzi wa mara kwa mara wa saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kuokoa maisha.

Aidha, Rais Samia amewataka wataalamu wa afya kuendelea kuimarisha kampeni za elimu kwa jamii, huku akipendekeza kuwepo kwa siku maalum za uchunguzi wa afya kwa wananchi, viongozi wa dini na wadau mbalimbali ili kuongeza upatikanaji wa huduma hizo.

Pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, taasisi za dini na vyombo vya habari katika kutoa elimu sahihi kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, ili kupunguza ushawishi wa tiba zisizo za kisayansi ambazo huchelewesha wagonjwa kupata matibabu sahihi.

“Imani na tiba si maadui. Mwenyezi Mungu ametupa maarifa na wataalamu kwa ajili ya kuokoa maisha. Tuwahimize wagonjwa kutumia huduma za kitaalamu,” alisema.

Ufunguzi wa jengo hilo la tiba ya mionzi unatajwa kuwa hatua muhimu katika kuboresha huduma za saratani nchini, ukilenga kupunguza safari ndefu za wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya kanda na kuongeza nafasi ya matibabu ya mapema na bora.

error: Content is protected !!