Rais Samia Suluhu Hassan ameziagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) kufuatilia miradi ya maendeleo iliyobainika kuwa na dosari na kuwachukulia hatua wahusika.
Rais Samia ameyasema hayo kwenye hafla ya Maadhimisho ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, kumbukumbu ya Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere na Wiki ya Vijana iliyofanyika katika Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera leo (14, Oktoba 2022).
Rais Samia amesema vitendo vya rushwa havivumiliki na mapambano ya dhidi ya vitendo hivyo ni lazima yaendelee.
“Hatuwezi kuvumilia uzembe na kutokuwajibika kunakosababishwa na vitendo vya rushwa na ufisadi,” amesema Rais Samia.
Sambamba na hilo taasisi hizo zenye kupambana na rushwa nchini zimeagizwa kuwachukulia hatua wasimamizi wa miradi iliyobainika kuwa na ufujaji, wizi, matumizi mabaya ya fedha, pamoja na rushwa.
Agizo hilo la Rais Samia limekuja mara baada ya kuwepo kwa vitendo vya rushwa kwenye miradi mbalimbali nchini hali inayopelekea miradi hiyo kutofikia viwango vinavyotakiwa.
“Kama Taifa bado tunaendelea kutafunwa na vitendo vya rushwa na ufisadi ambavyo ni adui mkubwa wa maendeleo,” amesema Rais Samia.