Rais Samia azindua maghala na vihenge Rukwa, aahidi uboreshaji wa sekta ya kilimo

HomeKitaifa

Rais Samia azindua maghala na vihenge Rukwa, aahidi uboreshaji wa sekta ya kilimo

Leo, Rais Samia Suluhu Hassan amezindua maghala ya kuhifadhi nafaka mkoani Rukwa, katika jitihada za kukuza sekta ya kilimo nchini. Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia alisema, “Tumekuja kuzindua maghala haya ya kuhifadhi nafaka. Lengo letu serikali ni kukuza sekta hii ya kilimo na kama mnavyosikia mwaka hadi mwaka tunaongeza bajeti ya kilimo ili tutoe huduma nyingi zaidi kwa wakulima na wakulima walime kwa wingi zaidi ili tuuze nje kwa wingi zaidi.”

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt, Samia Suluhu Hassan leo Julai 16,2024 amezindua Vihenge, Maghala ya kuhifadhi Chakula ya NFRA na msimu wa ununuzi wa nafaka eneo la Konondo Halmashauri ya Sumbawanga Mkoani Rukwa wakati wa Ziara ya Kikazi Mkoani humo.

Rais Samia alisifu juhudi za wakulima wa Rukwa, akisema, “Mkoa huu wa Rukwa ni kanda pekee inayojitegemea katika kilimo, manunuzi na uhifadhi wa nafaka, na hii ni kwa sababu wakulima ndugu zangu wa Rukwa mnalima kwa juhudi kubwa.”

Akifafanua zaidi kuhusu uwekezaji wa serikali katika mkoa wa Rukwa, Rais Samia alisema, “Katika mkoa huu tumemimina fedha nyingi sana za kilimo. Tunaleta mbolea ya ruzuku, kwa maana hiyo hata matumizi ya mbolea yameongezeka. Ukiangalia matumizi ya mbolea miaka 2 nyuma ni tofauti. Wakulima mnatumia mbolea nyingi sana kwa sababu mbolea inakuja kwa ruzuku, tutaendelea kutoa ruzuku.”

Muonekano wa Maghala na Vihenge mkoani Rukwa

Rais Samia pia alieleza kuhusu ujenzi wa miundombinu ya kumwagilia maji ili kuongeza uzalishaji wa mazao. “Tunajenga miundombinu ya kumwagilia ili wakulima muweze kulima mara mbili kwa mwaka, kwa maeneo mengine hata mara tatu lakini hasa mara mbili ili tuongeze uzalishaji na tukuze biashara ya mazao ya kilimo.”

Kuhusu huduma za ugani, Rais Samia alisema, “Huduma za ugani nazo tumeziboresha sana. Tunapima afya ya udongo na huduma nyingine za ugani tunaziboresha.”

Rais Samia alieleza umuhimu wa maghala na vihenge vipya kwa wakulima. “Tunajenga vihenge na maghala ili wakulima mnapovuna basi tuweze kununua serikali na kuhifadhi kwa haraka.”

Akiendelea, Rais Samia aliongeza kuwa serikali imeipa nguvu NFRA kwa kuongeza uwezo wa kifedha, kiutendaji, na kiteknolojia. “Kama mnavyoona tumekuza teknolojia kwenye upimaji wa ubora lakini tumekuza teknolojia kwenye ununuzi kuharakisha ununuzi na kuondoa dhurma zilizokuwa zikifanyika nyuma.”

Kuhusu bei ya nafaka, Rais Samia alisema, “Kulikua na kilio cha bei, tumeongeza tumesema vijijini tutanunua kwa 600, mjini tutanunua kwa 650 kwa kilo, lakini tutaangalia hali inavyokwenda kama tutaweza kuongeza bei basi tutaongeza bei.”

Hatua hizi zote ni sehemu ya mpango mpana wa serikali wa kuhakikisha ustawi wa sekta ya kilimo na kuinua maisha ya wakulima nchini.

 

 

error: Content is protected !!