Utafiti: Nusu ya mimba duniani hazikutarajiwa

HomeMakala

Utafiti: Nusu ya mimba duniani hazikutarajiwa

Ripoti mpya ya idadi ya watu inaeleza kuwa karibu nusu ya mimba zinazotungwa kila mwaka duniani zinakuwa siyo za kutarajiwa ambapo husababishwa na ukosefu wa elimu ya uzazi na matumizi duni ya njia za uzazi wa mpango. 

Mimba hizo hujumuisha wasichana wanaopata katika umri mdogo, jambo linalowafanya wakatize masomo.

Ripoti ya Hali ya Idadi ya Watu Duniani mwaka 2022, iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na idadi ya watu na afya ya uzazi (UNFPA) imesema karibu nusu ya mimba zote milioni 121 zinazotungwa kila mwaka duniani kote, hazikutarajiwa.

Ripoti hiyo ya “Kuona Yasiyoonekana: Kuchukua hatua katika janga lililopuuzwa la mimba zisizotarajiwa,” imezinduliwa jijini New York Marekani ambapo imeeleza kuwa kwa wanawake na wasichana walioathiriwa na mimba zisizotarajiwa, chaguo hili kubwa zaidi la uzazi maishani la kuwa iwapo wanataka kuwa na ujauzito au la huwa siyo chaguo lao binafsi.

“Ripoti hii ituamshe kutoka usingizini. Idadi kubwa ya mimba zisizotarajiwa inaonesha kushindwa duniani kote kutetea haki za msingi za wanawake na wasichana,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Dk Natalia Kanem.

UNFPA imeonya kwamba mgogoro huu wa haki za binadamu una madhara makubwa kwa jamii, kwa kuwa zaidi ya asilimia 60 ya mimba zisizotarajiwa huishia katika utoaji mimba na inakadiriwa asilimia 45 ya mimba zote si salama ambapo husababisha asilimia 5 mpaka 13 ya vifo vya uzazi.

Athari hizo huathiri uwezo wa dunia kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya mwaka 2030.

Ukosefu wa usawa wa kijinsia na maendeleo huchangia kwa viwango vya juu kwa wanawake na wasichana kupata mimba zisizotarajiwa ulimwenguni kote.

Inakadiriwa kuwa wanawake milioni 257 ambao wanataka kuepuka mimba hawatumii njia salama na za kisasa za uzazi wa mpango. 

Katika maeneo ambapo takwimu hazikupatikana, karibu robo ya wanawake wote hawatumii njia salama za uzazi wa mpango. Jingine kubwa lililobainika ni wanawake kutokuwa na uwezo wa kusema hapana kwa ngono.

Sababu nyingine zinazochangia:

  •  Ukosefu wa taarifa za huduma ya afya ya ngono na uzazi 
  •  Njia za uzazi wa mpango ambazo haziendani na miili ya wanawake au hali zao
  •  Mtazamo wa kuhukumu au aibu katika kupata huduma za afya
  • Umaskini na maendeleo ya kiuchumi yaliyokwama

Nini kifanyike?

Ripoti hiyo inapendekeza watoa maamuzi na mifumo ya afya kuweka kipaumbele katika uzuiaji wa mimba zisizotarajiwa kwa kuboresha upatikanaji wa aina mbalimbali za uzazi wa mpango na kupanua kwa kiasi kikubwa huduma bora ya afya ya ngono na taarifa za masuala ya uzazi wa mpango. 

Watunga sera, viongozi wa jamii na watu wote wamehimizwa kuwawezesha wanawake na wasichana kufanya maamuzi kuhusu ngono, uzazi wa mpango na uzazi kwa ujumla, na kuhakikisha wanakuza jamii zinazotambua thamani kamili ya wanawake na wasichana kwakuwa wakifanya hivyo wataweza kuchangia kikamilifu katika jamii, na watakuwa na zana, taarifa na uwezo wa kufanya maamuzi yao wenyewe.

Kupata maelezo zaidi tembelea tovuti ya  www.unfpa.org 

 

error: Content is protected !!