Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema ili nchi ifikie malengo iliyojiwekea katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, taasisi za umma, sekta binafsi na wananchi wanapaswa kuwa na mabadiliko ya fikra, utendaji kazi pamoja na mifumo.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza na Watanzania katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika jijini Dodoma Julai 17, 2025, amesema dira hiyo inalenga kuifikisha Tanzania katika ngazi ya uchumi wa kati wa juu ifikapo mwaka 2050.
Rais Samia amesema lengo hilo litafikiwa kwa kufikia pato la Taifa la Dola Trilioni moja za Marekani na pato la mtu mmoja mmoja la zaidi ya Dola 7,000 za Marekani kwa mwaka.
“Hatutoweza kufikia lengo hili kama tutaendelea kufanya kazi kwa mazoea. Lazima tubadilike kifikra, kimtazamo na kimatendo. Vile vile lazima tupimane kwa matokeo ya kazi,” ameeleza Rais Samia.
Kwa mujibu wa Benki ya Dunia (WB) Tanzania kwa sasa ni nchi ya kipato cha kati cha chini, ikiwa na pato la taifa kwa mtu mmoja (GDP per capita) la Dola za Marekani 1,149 sawa na Sh2.9 milioni.
Katika kuhakikisha utekelezaji wa dira hiyo, Rais Samia ameielekeza Tume ya Taifa ya Mipango, kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, kuandaa nyenzo zitakazopima utendaji wa serikali kulingana na malengo ya dira.
Ameagiza pia sera zote za wizara zipitiwe na kurekebishwa kabla ya utekelezaji kuanza rasmi Julai 2026.
Rais pia ameitaka Tume hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanza mchakato wa kuchambua na kupendekeza maboresho ya kisheria ili kuwezesha utekelezaji wa dira.
Aidha, mfumo wa ufuatiliaji na tathmini umetajwa kuwa kipaumbele katika kuhakikisha taasisi zote za umma zinapimwa kwa vigezo maalum vinavyolingana na malengo ya dira.
Rais Samia ameelekeza pia taasisi za Serikali kuwa na viashiria vya utendaji vinavyoendana na dira hiyo.
Kwa upande wa sekta binafsi, Rais Samia amesema mafanikio ya dira hayawezi kufikiwa bila ushiriki wa dhati wa sekta hiyo ambapo ameitaka sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika maeneo ya kiuchumi, uwekezaji, ubunifu, uundaji wa ajira zenye staha na kuongeza tija.