Rais Samia : Hongereni wakulima, wafugaji na wavuvi

HomeKitaifa

Rais Samia : Hongereni wakulima, wafugaji na wavuvi

Rais Samia Suluhu Hassan amewapongeza wakulima, wafugaji, na wavuvi kwa juhudi zao kubwa zinazochangia katika maendeleo ya sekta ya kilimo, mifugo, na uvuvi nchini. Akizungumza kwenye kilele cha Maonesho ya Nanenane yaliyofanyika Dodoma, Rais Samia alionyesha kufurahishwa na maandalizi ya mabanda na mabadiliko makubwa yaliyofanywa kwenye uwanja wa maonesho.

“Nimejiona na kujifunza mambo mengi katika muda huo, mabanda yameandaliwa vizuri sana na yana mambo mengi sana. Hongereni sana,” alisema Rais Samia huku akitoa pongezi kwa Wizara ya Kilimo kwa maandalizi mazuri.

Rais Samia Suluhu akiwa kwenye moja ya banda lililokuwepo kwenye Maonesho ya Nanenane mkoani Dodoma.

Rais Samia alibainisha kuwa wakati anaelekea kwenye maonesho hayo, hakuwa na picha kamili ya mabadiliko yaliyofanywa kwenye uwanja wa maonesho, lakini alifurahishwa sana na hali aliyokutana nayo. “Nilivyoingia nimefurahishwa sana na mabadiliko yanayoendelea. Hongereni sana Wizara,” aliongeza.

Aidha, Rais Samia aliwatia moyo waliohudhuria maonesho hayo kwa kusema kuwa anaamini waliopata fursa ya kujifunza katika kipindi hicho watarejea na maarifa mapya yatakayosaidia kuboresha shughuli zao za kilimo, mifugo, na uvuvi katika maeneo yao.

Akirejelea ziara zake za hivi karibuni mkoani Katavi, Rukwa na Morogoro, Rais Samia alieleza jinsi alivyowashukuru wakulima wa mikoa hiyo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kulilisha taifa. “Niliwashukuru wakulima wa mikoa hiyo na kupitia kwao kuwashukuru wakulima nchini kote…Niliwashukuru kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kulilisha taifa na kutupa uhakika wa chakula,” alieleza.

Rais Samia alitumia jukwaa hilo kuwashukuru na kuwapongeza wakulima, wafugaji, na wavuvi kwa juhudi zao ambazo zimeiwezesha Tanzania kufikia kiwango cha utoshelezu wa chakula kwa asilimia 128. “Jasho na juhudi zenu zina thamani kubwa sana katika nchi yetu,” alisema huku akisisitiza dhamira ya serikali yake ya kujenga uchumi jumuishi unaowainua wananchi wote na kuwawezesha kunufaika ipasavyo na jasho lao.

Kwa kumalizia, Rais Samia alihimiza ushirikiano kati ya sekta zote ili kuhakikisha mafanikio zaidi yanapatikana katika sekta ya kilimo, mifugo, na uvuvi, akisisitiza kuwa mchango wa wakulima, wafugaji, na wavuvi ni muhimu katika kuhakikisha taifa linakuwa na uhakika wa chakula na malighafi za viwandani.

 

 

 

error: Content is protected !!