Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema sasa jicho la Serikali lipo katika wizara mpya iliyoundwa ya Mipango na Uwekezaji ambapo itakuwa na majukumu makuu matatu ikiwemo kutafuta fursa za uwekezaji nchini.
Wizara hiyo mpya ambayo ipo chini ya Ofisi ya Rais itakuwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Tume ya Mipango pamoja na Uwekezaji.
Rais Samia aliyekuwa akiwaapisha viongozi aliwateua Julai 5 2023, Ikulu jijini Dar es Salaam, amemwambia Kitila Mkumbo ambaye ni waziri wa wizara hiyo mpya kuwa, Tanzania bado haifanyi vyema kwenye kutumia fursa za uwekezaji akitolea mfano suala la bandari ya Dar es Salaam.
“Wakati sisi tunalumbana bandari apewe nani, wenzetu kwa kuona malumbano yetu wamekimbia wameenda kule kule, wakati Bunge linaridhia kuendesha bandari ya Dar es Salaam wenzetu wamesema zote wanaipatia sekta binafsi,” amesema Rais Samia leo Julai 14.
Rais Samia amesisitiza kuwa kinachotokea ni mfano halisi wa namna fursa zinavyoweza kupotea haraka hivyo ni wajibu wa wizara hiyo kuhakikisha fursa zinafanyiwa kazi ipasavyo.
Mwelekeo wa nchi kubadilishwa
Kwa Mujibu wa Rais Samia jukumu la pili la wizara hiyo ni kubadili mwelekeo wa nchi kulingana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia na mazingira ya sasa ili nchi iweze kupiga hatua katika maendeleo.
“Hapa pana kazi kubwa kweli kweli lakini kwenye nia safi na ya kujenga nchi, msiogope kuja na mawazo ya kubadilisha mwelekeo wa nchi, kila mabadiliko yana ugumu wake, hakuna mabadiliko rahisi,” amesisitiza Rais Samia.
Aidha, kutokana na Tanzania kuwekeza zaidi kwenye mipango imayohusisha masuala ya kifedha pekee, wizara hiyo itakuwa na wajibu wa kusimamia na kuendeleza rasilimali watu kwa kuzingatia mwelekeo wa dunia kwa sasa.
Ili kuwezesha hilo wizara hiyo itatakiwa kupitia mitaala mipya ya elimu na kushauri mwelekeo wa rasilimali watu ambapo mfumo wa elimu wa sasa umekuwa ukipigiwa kelele kuwa unazalisha wategemezi zaidi.
Kuundwa kwa Wizara hiyo kunatokana na kupitishwa kwa Sheria ya Tume ya Mipango ya mwaka 2023 ambapo pamoja na mambo mengine, tume hiyo itakuwa na jukumu la kubuni, kupanga, kuratibu na kusimamia mipango ya maendeleo ili kuwa na mfumo jumuishi wa ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa vipaumbele vya maendeleo ya Taifa.