Magari haya yanatumia kiwango kidogo cha mafuta

HomeElimu

Magari haya yanatumia kiwango kidogo cha mafuta

Bei za mafuta zimeendelea kupaa katika soko la dunia na Tanzania, jambo lililosababisha gharama za maisha kuongezeka kwa kasi.

Hii imewafanya baadhi ya wamiliki wa magari yanayotumia mafuta kuanza kutafuta njia mpya ya kuokoa shilingi zao.

Ingawa matumizi ya mafuta kwenye gari  hutegemeana na sababu mbalimbali ikiwemo hali ya barabara, namna ya uendeshaji pamoja na sifa za kiufundi za gari husika, njia mojawapo ya kuepusha mfuko kutoboka zaidi ni kutumia magari yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta.

Kwa mujibu wa  maelezo ya wataalamu wa magari wakiwemo mafundi na wale wanaojihusisha na uagizaji na uuzaji wa magari kutoka nje ya nchi ufuatao ni  mchanganuo wa magari yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta kulingana na kampuni zao.

1.Toyota IST

Hii ndiyo gari iliyoonekana kupendwa zaidi na Watanzania hususani wa  maeneo ya mjini kutoka kampuni ya Toyota. Kwa mujibu wa kampuni ya usafirishaji wa magari kutoka nchini Japan  mpaka Tanzania ya FORWARD JP, gari hilo ni chaguo namba moja katika kutumia mafuta kidogo

Sababu zinazotajwa ni pamoja na kuwa gari inayotosha kwa familia ndogo ya mijini ikiwa na nafasi ya ziada kwenye buti,uimara wake barabarani, na  sababu kubwa zaidi ni matumizi madogo ya mafuta.

Zipo aina mbili za injini ya gari ya IST ambazo ni yenye cc1300 2NZ-FE 14 ambayo hutembea kilomita 18.2 kwa lita moja ya mafuta na yenye cc1400 1NZ-FE 14 hutembea kilomita 16 kwa lita moja.

Cc huumanisha uwezo wa injini ya gari.

2.Toyota Ractics 

Jina la gari hii limetokana na sifa kuu tatu ambazo ni uwezo wa kukimbia, utendaji wake wa kazi pamoja na nafasi (run, activity, space).

Ikiwa na tenki yenye uwezo wa kuhifadhi lita 42 za mafuta, gari hii ina uwezo wa kutembea kilomita 18.2 kwa lita moja kwa gari yenye injini ya cc1300 na kilomita 15.2 kwa gari yenye injini ya cc1500 kwa mujibu wa BE FORWARD.

3.Toyota Passo

Gari hii ina aina mbili za injini mojawapo ni yenye cc1000 na yenye cc1300. Kwa mujibu wa TCV, kampuni ya kimataifa ya uuzaji wa magari, gari hii imefikia kiwango cha mwaka 2005 cha kupunguza kiwango cha gesi ya kutolea nje kwa asilimia 75 na kuthibitishwa na mamlaka za Japan.

Gari hili Ni bora kwa wale ambao wana familia ndogo na bajeti ndogo kwani matumizi ya mafuta yameboreshwa kutokana na mpangilio wa jumla wa injini ya Toyota Passo inasaidia matumizi bora ya mafuta ambapo  ina uwezo wa kutembea kilomita 17 kwa lita moja.

4.Toyota Vitz.

Mnamo mwezi Disemba mwaka 2010 kampuni ya Toyota ya nchini Japan ilitangaza kuingiza sokoni gari aina ya Toyota Vitz baada ya kukamilisha maboresho ya gari hiyo.

Ikiwa na injini yenye ukubwa wa cc1300 gari hiyo ilitajwa kuwa na  uwezo wa kutembea kilomita 26 kwa lita moja nchini Japan.

Hata hivyo, kumekuwa na mjadala kuhusu uwezo wa gari hii kutumia kiasi kidogo cha mafuta. Hilo linategemea hali ya gari, namna gari inavyo endeshwa, injini ya gari pamoja na mazingira.

Katika mazingira ya Afrika gari hii ina uwezo wa kutembea kati ya  kilomita 8.9 mpaka kilomita 21.5 kwa lita moja  kutegemeana na sababu tajwa hapo juu.

5. Toyota Raum

Gari hii inayotumia mafuta ya petroli mara nyingi huwa na injini yenye ukubwa wa cc1500 yenye nguvu ya hp 109(uwezo wa gari kwenda kasi),spidi ya juu ya kilomita 170 pamoja na tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 45 za mafuta ambapo hutumia lita 1 kwa kilomita 16.2

Kwa mujibu wa BE FORWARD GP, magari yanayozalishwa na kampuni ya Toyota yananunuliwa zaidi nchini Tanzania kutokana na unafuu wake pamoja na upatikanaji rahisi wa vifaa vyake pale yanapoharibika.

6.Subaru Impreza 

Kampuni ya Subaru ya nchini Japan, imekuwa ikizalisha gari hili tangu mwaka 1992 katika mitindo yote miwili ya Sedan na Hatch ambayo yamekuwa yakifayiwa marekebisho na maboresho na toleo la mwisho ni la mwaka 2021.

Gari hili lina injini yenye ukubwa wa cc1498 na matumizi yake ya mafuta ni wastani wa  kilomita 12.7 kwa lita moja lakini umbali unaweza kuongezeka au kupungua kutegemeana na sababu nyinginezo na hii ni  mujibu wa tovuti ya uuzaji wa magari ya One Shift ya nchini Singapore.

7.Suzuki Jimny

Gari hii ni mfululizo wa matoleo ya  magari i yenye injini ya  kusukuma magurudumu manne tangu mwaka 1970 yanayozalishwa na kampuni ya Suzuki.

Pamoja na Suzuki kuwa na aina nyingine za magari, yanayosifika kwa kupita katika barabara mbaya (off road), gari hii imeonekana kupendwa zaidi ambapo kwa mujibu wa Suzuki mwaka 2018 gari hiyo ilikuwa imeshauzwa katika nchi 194 duniani.

Gari hili lenye milango miwili, lina injini yenye uwezo wa cc1500 yenye kutumia lita moja kwa kilomita 13 hadi 16, kwa mujibu wa TVC.

error: Content is protected !!