Rais Dk Samia Suluhu Hassan amewasili Addis Ababa kufanya ziara ya kikazi kuanzia leo hado Februari 16, kushiriki Mkutano wa Kawaida wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU).
Taarifa ya Ikulu imesema mkutano huo unatarajia kuchagua Mwenyekiti Mpya wa Umoja wa Afrika kwa mwaka 2025 atakaechukua nafasi ya Mwenyekiti wa sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Mauritania.
Aidha, mkutano huo pia utachagua viongozi wapya wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika wakiwemo Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Makamishna sita.
Vilevile, mkutano utajadili taarifa ya ushiriki wa Umoja wa Afrika kwenye Mkutano wa Nchi Tajiri Duniani (G20), Utekelezaji wa Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika na taarifa kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabianchi.
Mbali na masuala hayo, mkutano utajadili ajenda kuhusu matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia iliyopendekezwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kabla ya kushiriki mkutano wa 38, Rais Dk Samia atashiriki Mkutano wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika utakaofanyika leo.