Rais Samia kujenga chuo cha masuala ya anga Tanzania

HomeKitaifa

Rais Samia kujenga chuo cha masuala ya anga Tanzania

Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali ina mpango wa kujenga chuo cha masuala ya anga nchini Tanzania kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga cha Korea.

Rais Samia alitoa kauli hiyo wakati wa hafla ya kutunukiwa Shahada ya Udaktari wa Falsafa wa Heshima (Honoris Causa) katika sekta ya anga na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga (Korea Aerospace University).

Alisema sekta ya anga ya Tanzania imekua kati ya mwaka 2021 na 2023, ambapo idadi ya abiria imeongezeka kwa takriban asilimia 28 kila mwaka na idadi ya ndege zinazofanya safari za kimataifa imeongezeka kutoka 26 hadi 33.

Aidha, idadi ya wasafiri wa ndani imeongezeka kwa asilimia 26.5 baada ya janga la Covid-19, kutoka abiria milioni 3 hadi kufikia milioni 3.8 kwa mwaka 2023.

Rais Samia alisema nia ya Serikali ilikuwa kuwekeza kimkakati, hasa katika kufufua kampuni ya Air Tanzania Limited (ATCL) na kuendeleza miundombinu, ikiwemo mfumo wa kujenga rada na pia kukarabati na kupanua viwanja vya ndege kote nchini. Kabla ya mwaka 2016, ATCL ilikuwa na ndege moja inayofanya kazi, lakini kufikia Machi 2024 imeongeza ndege 14 za abiria na moja ya mizigo.

error: Content is protected !!