Balozi Togolani akanusha taarifa za kutolewa kwa sehemu ya bahari kwa mkopo

HomeKitaifa

Balozi Togolani akanusha taarifa za kutolewa kwa sehemu ya bahari kwa mkopo

Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Togolani Mavura, amethibitisha kuwa Tanzania haikusaini mkataba wowote na Jamhuri ya Korea kuhusu Bahari ya Tanzania au Madini wakati wa ziara ya Rais Samia Suluhu nchini Korea.

Balozi Mavura ameeleza kuwa katika ziara hiyo iliyozinduliwa Mei 31, 2024, Rais alishuhudia tu utiwaji saini wa mkataba mmoja, ambao ni mkataba wa mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 2.5 kwa miradi ya miundombinu.

Mbali na mkataba huo, alisema Rais Samia alishuhudia pia utiwaji saini wa Hati mbili za Makubaliano (Memorandum of Understanding-MOU) kwa ushirikiano katika Sekta ya Uchumi wa Buluu na Madini ya Kimkakati.

Zaidi ya hayo, Rais pia alishuhudia utiwaji saini wa Tamko la Kuanzisha Majadiliano ya Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi (Joint Statement on the launch of Negotiation on Economic Partnership Agreement-EPA).

“Tanzania na Korea wamesaini mkataba mmoja; Hati mbili za Makubaliano, na Tamko moja,” alisema Balozi Mavura.

Aidha, alifafanua kuwa Tanzania haijatoa chochote kama fidia kwa mkopo nafuu kutoka Korea kama ilivyodaiwa kwenye mitandao ya kijamii. Badala yake, Tanzania inapokea mkopo nafuu kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo (EDCF) kwa mara ya tatu.

“Mara ya kwanza ilikuwa dola milioni 733 (2014-2020); mara ya pili dola bilioni 1 (2021-2025), na huu wa tatu ni dola bilioni 2.5 (2024-2028),” alieleza, akiongeza kuwa “nchi 59 barani Afrika, Asia, na Ulaya zinawanufaika na mkopo huu kutoka EDCF.”

Balozi Mavura alisisitiza kuwa “mkopo huu wa masharti nafuu una riba ya asilimia 0.01, unalipwa kwa miaka 40, na una kipindi cha kutoa (grace period) cha miaka 25, maana yake marejesho yanaanza baada ya mwaka wa 26. Kwa hivyo, si kweli kwamba mkopo utalipwa kwa miaka mitano.”

error: Content is protected !!