Rais Samia: Uchumi wetu ni himilivu

HomeKitaifa

Rais Samia: Uchumi wetu ni himilivu

Rais Samia Suluhu Hassan ameelezea mafanikio makubwa ambayo Tanzania imeyapata katika kuimarisha uchumi na kutengeneza mazingira bora ya uwekezaji na biashara. Akizungumza katika mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara Tanzania (TNBC), Rais Samia alisisitiza dhamira ya serikali ya kuhakikisha kuwa nchi inabaki kuwa na uchumi imara unaovutia wawekezaji na wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi.

“Napenda kuwafahamisha kuwa pamoja na changamoto mbalimbali tunazozishuhudia kwenye uchumi wa dunia, uchumi wetu wa Tanzania umekuwa himilivu na umeendelea kukua na kuimarika zaidi,” alisema Rais Samia.

Kwa mujibu wa vigezo vya kimataifa (Global Credit Rating), Tanzania imeendelea kuwa na uchumi wa kati uliochanya na imara, ambapo imepata alama ya B+, kiwango ambacho ni bora zaidi kuliko mwaka 2022. Hali hii nzuri ya kiuchumi imewezesha Tanzania kukuza biashara na kuvutia uwekezaji zaidi, jambo lililopelekea ongezeko la miradi ya uwekezaji.

Rais Samia alifafanua zaidi kuhusu mafanikio haya, akisema: “Mwaka 2023, uchumi wetu ulikua kwa asilimia 5.2 ikilinganishwa na asilimia 4.7 mwaka 2022. Vilevile, mfumuko wa bei umeendelea kubaki asilimia 3 ndani ya lengo letu [asilimia 3 mpaka 5] na utoshelevu wetu wa chakula ni zaidi ya asilimia 120.”

Kwa juhudi za kuendelea kuvutia wawekezaji, Rais Samia alitangaza mageuzi makubwa katika sekta ya reli kwa kuondoa ukiritimba katika uendeshaji wa shughuli za reli nchini. Serikali, ikiongozwa na falsafa ya R4, imerekebisha sheria ya reli ili kuruhusu waendeshaji binafsi kutumia miundombinu hiyo kutoa huduma za usafirishaji.

“Niwataarifu kwamba, tukiongozwa na falsafa ya R4, Serikali imekuja na mageuzi ya kuondoa ukiritimba katika uendeshaji wa shughuli za reli. Tumerekebisha sheria ya reli ili kuruhusu waendeshaji binafsi kutumia miundombinu hiyo kutoa huduma za usafirishaji,” alisema Rais Samia.

Rais Samia pia alionyesha jinsi wigo wa kukopa na kukopeshwa kwa serikali na makampuni umeongezeka wakati riba zimeendelea kubakia katika viwango vya kuridhisha, hali inayosaidia zaidi katika ukuaji wa uchumi na uwekezaji.

Kwa ujumla, mkutano wa TNBC ulionesha kuwa Tanzania inaendelea kufanya mageuzi muhimu na kuimarisha uchumi wake, huku ikitoa fursa zaidi kwa sekta binafsi kushiriki katika uendeshaji wa miundombinu na huduma mbalimbali. Hii inalenga kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara zaidi kwa manufaa ya Taifa na wananchi wake.

 

 

error: Content is protected !!