Rais Samia : Wakuu wa Mikoa ni marais katika maeneo yenu

HomeKitaifa

Rais Samia : Wakuu wa Mikoa ni marais katika maeneo yenu

Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wakuu wa mikoa nchini kutatua changamoto za wananchi, ikiwemo migogoro ya ardhi pamoja na kuongeza ukusanyaji wa mapato yatakayochangia pato la Taifa na upatikanaji wa huduma za kijamii.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika hafla ya kuwaapisha wakuu wa mikoa wapya leo Machi 13, 2024 jijini Dar es Salaam amesema wakuu wa mikoa ndio watatuzi wakubwa wa matatizo yanayowakumba wananchi katika maeneo waliyopewa kuongoza.

“Nataka niwakumbushe nyinyi ndio maraisi wa maeneo yale, shida yoyote ya maeneo yale ni shida yako…kuna Maras (Makatibu Tawala wa mikoa) na Madas ( Makatibu Tawala wa Wilaya ) hao wote wamewekwa wakusiadieni, mpaka apite Makonda watu walie? Hivyo sivyo,”amesema Rais Samia.

 

Maagizo ya kiongozi huyo yamekuja wakati ambapo kuna vuguvugu la malalamiko ya mbalimbali ya wananchi ikiwemo migogoro ya ardhi, ubovu wa miundombinu, na huduma za kijamii kutoka kwa wananchi.

Kutokana na kutosikilizwa na viongozi wao kwa ngazi za wilaya na mikoa siku za hivi karibuni wananchi hao wamekuwa wakiwasilisha malalamiko yao kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Paul Makonda kupitia ziara zake anazofanya katika mikoa mbalimbali.

 

Rais Samia amewaambia wakuu wa mikoa kuwa kutowasikiliza wananchi kunawafanya baadhi yao kukosa imani na Serikali iliyopo madarakani jambo linaloweza kuathiri uchaguzi wa Serikali za mitaa na madiwani mwakani na uchaguzi mkuu mwaka 2025.

“Wasiposikilizwa zile ndizo kura zetu, akipita mwingine akiwaambia mie nikiingia nitawasikiliza watampa kwa sababu sisi tumewapuuza hatuwasilikizi, kule ndipo ulipo ushindi wa chama kilichowawekeni madarakani…niwasisitize sanaa kuwasiliza wananchi,” amesema Rais Samia.

Mbali na maagizo hayo Rais Samia amesisitiza suala la ukusanyaji wa mapato ambalo kwa baadhi ya halmashauri bado lipo nyuma licha ya kupokea fedha nyingi za maendeleo.

Aidha, amewataka viongozi hao wateule wa mikoa walioapa leo na wale ambao wapo madarakani kusimamia lishe kwa kuzalisha mazao ya kutosha ya chakula, usimamizi wa fedha pamoja na kupuguza migogoro isiyo ya lazima baina yao na viongozi wengine.

error: Content is protected !!