Rais Samia: Walidhamiria kuipindua nchi Oktoba 29

HomeKitaifa

Rais Samia: Walidhamiria kuipindua nchi Oktoba 29

Rais Samia Suluhu Hassan amesema kulikuwa na jaribio la kuipindua nchi na kuondoa dola iliyopo madarakani katika maandamano yaliyofanyika siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, na kusababisha vifo vya watu na uharibifu wa mali za umma na binafsi.

Katika hotuba yake kwa wazee wa Dar es Salaam pamoja na kuhutubia Taifa leo Desemba 2, 2025, Rais Samia amesema tukio hilo ni la “kutengeneza na waliotengeneza walidhamilia makubwa.”

Kauli ya Rais Samia inakuja ukiwa umepita takriban mwezi mmoja tangu, tukio hilo litokee na tayari ameshaunda tume ya kuchunguza kiini cha tukio hilo ikiwemo kubaini mzizi wa kilichosababisha vijana kuingia barabarani kwa ajili ya maandamano.

“Walidhamiria kuangusha dola ya nchi yetu,” amesema Rais Samia akibainisha kuwa vijana “walifanywa makasuku” na kuimbishwa kuwa yaliyotokea Madagascar yatokee na Tanzania bila kujua undani wa jambo hilo lililotokea katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.

Tukio hilo, amesema, ni mradi mkubwa wenye nia ovu ambao una wafadhili, washitiri, pamoja na watekelezaji lililowahusisha watu waliodhamiria kuhujumu Serikali huku wengine wakifuata mkumbo.

Rais Samia amesema kilichofanyika si maandamano bali ni vurugu kwa kuwa maandamano yanayokubalika kisheria ni lazima yawe na kibali na yaeleze yatapita wapi, kisha kuwe na ulinzi wa askari polisi wataosimamia usalama wao.

error: Content is protected !!