Rais Samia: Watumishi watumikieni wananchi

HomeKitaifa

Rais Samia: Watumishi watumikieni wananchi

RAIS Samia Suluhu Hassan amewakumbusha watumishi wa umma kote nchini kuwa wamekasimiwa majukumu ya kuwatumikia wananchi na amewataka wasimame ipasavyo katika nafasi zao na kutimiza majukumu yao.

Ametoa msisitizo huo leo wakati akizungumza na wananchi na watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Handeni mara baada ya kufungua rasmi Jengo la Halmashauri hiyo.

Aidha, Rais Samia ameeleza imani yake kuwa jengo hilo linaimarisha utawala bora na huduma kwa wananchi. Jengo hilo ni moja kati ya majengo 122 yaliyojengwa katika Halmashauri mbalimbali nchini tangu mwaka 2021 ikiwemo jengo la Halmshauri ya Wilaya ya Bumbuli ambalo Rais Dkt. Samia amelizindua jana tarehe 24 Februari, 2025.

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wananchi wa Handeni kwenye mkutano wa hadhara katika muendelezo wa ziara yake ya kikazi mkoani Tanga tarehe 25 Februari, 2025.

Awali akiwa Wilaya ya Handeni, ameweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Maji wa Miji 28 unaoenda kuimarisha upatikanaji wa maji katika Wilaya za Handeni, Korogwe, Muheza na Pangani.

Mradi wa Maji wa Miji 28 Tanga uliekewa Jiwe la Msingi na Rais Samia Suluhu Februari 25, 2025.

Katika hatua nyingine, akiwa Wilaya ya Kilindi, Rais Samia ametambua mchango uliotolewa na marehemu Beatrice Shelukindo wakati wa uhai wake katika kutetea haki za wanawake na kupitia nafasi za uongozi alizozishika ikiwemo Ubunge wa Jimbo la Kilindi na Mbunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa heshima yake, Rais Samia ameelekeza Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Tanga ipewe jina la Beatrice Shelukindo.

Muonekano wa Shule ya Sekondari ya Wasichana mkoa wa Tanga ambayo Rais Samia Suluhu ametoa pendekezo iitwe Shule ya Wasichana Sekondari Beatrice Shelukindo.

Shule hiyo ambayo Rais Samia ameizindua leo na inayojikita kwenye masomo ya sayansi ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kujenga shule 26 za wasichana katika kila Mkoa kwa lengo la kuimarisha ushiriki wa wanawake kwenye masomo ya sayansi.

Matukio yote hayo ni mwendelezo wa ziara ya wiki moja ya Rais Samia katika Mkoa wa Tanga.

error: Content is protected !!