Rais Samia: Wazazi waacheni watoto wasome

HomeKitaifa

Rais Samia: Wazazi waacheni watoto wasome

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi wa Ifakara na Mlimba kuhakikisha watoto wao wanapata elimu kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla. Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Ifakara, Rais Samia alieleza furaha yake kwa ongezeko la shule za msingi na sekondari katika maeneo hayo.

“Nafurahi kuwa Kilombero sasa ina shule za msingi 184, Mlimba 99 na Ifakara mjini 85, na shule za sekondari sasa ziko 55, Mlimba 26 na Ifakara mjini 29. Hizi ni shule nyingi sana, hongereni wana Mlimba na Ifakara,” alisema Rais Samia, akitoa pongezi kwa juhudi za ujenzi wa miundombinu ya elimu.

Rais Samia alisisitiza umuhimu wa elimu na kufafanua kuwa ingawa elimu ni bure kwa wazazi, gharama zake zinaendeshwa na serikali. “Tumejenga shule hizi nyingi sana lakini pia tumeondoa gharama kwa wazazi kusomesha watoto kwa jina la elimu bure. Lakini elimu hii niwaambie sio bure, ni elimu inayolipiwa na serikali,” alieleza Rais Samia, akiwataka wazazi kushirikiana na serikali kwa kuhakikisha watoto wao wanapata elimu.

Aliendelea kuwasihi wazazi kuachia watoto wao kuhudhuria shule na kufaidika na fursa zinazotolewa na serikali. “Niwaombe sana wazazi wenzangu waacheni watoto wakasome. Madarasa haya tunayoyajenga, shule tunazozijenga, walimu tunaoajiri ni kwa ajili ya watoto wetu hawa. Sasa waacheni watoto wakasome,” alisisitiza.

Katika jitihada za kuimarisha elimu ya ufundi na maarifa, Rais Samia alibainisha kuwa serikali imejenga vituo vya VETA kila wilaya ili kuwapa vijana ujuzi wa kujiajiri. “Tumeweza kujenga VETA kila wilaya, shule ambazo zinafanya elimu ya maarifa inawapa watoto amali za ujuzi wa kuweza kujiajiri au kuajiriwa,” alisema.

Rais pia alibainisha kuwa serikali inaendelea na juhudi za kujenga vituo vya VETA katika maeneo mengine nchini. “Nimewasikia wabunge wakisema kwenye maeneo yao VETA pia zinajengwa. Lengo kuu ni kuwafanya vijana wetu waweze kujiajiri na hasa sasa hivi umeme upo kila kona ya Tanzania,” alihitimisha Rais Samia.

Matamshi haya ya Rais Samia yanadhihirisha nia ya serikali ya kuwekeza katika elimu na kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata fursa sawa ya kupata elimu bora na ya kisasa, huku akisisitiza ushirikiano wa wazazi katika kufanikisha malengo hayo.

 

 

error: Content is protected !!