Sababu ya Rais Samia kuelekeza tuzo kwa Magufuli

HomeKitaifa

Sababu ya Rais Samia kuelekeza tuzo kwa Magufuli

Licha ya kupata tuzo ya heshima kuhusu ujenzi wa barabara barani Africa, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameelekeza tuzo hiyo kwa mtangulizi wake hayati Dk John Magufuli akieleza mafanikio yaliyopo katika ujenzi wa miundombinu ni matokeo ya kazi ya kiongozi huyo aliyefariki Machi 2021. 

Rais Samia ametunukiwa tuzo ya Babacar Ndiaye (mjenzi bora wa barabara) aliyokabidhiwa hii leo (Mei, 25 2022) nchini Ghana kutokana na mchango wake mkubwa katika ujenzi wa miundombinu nchini Tanzania.

Tuzo hiyo hutolewa kila mwaka na Jukwaa la habari kuhusu miundombinu na barabara Afrika (Acturoutes) na Shirika la Miundombinu na Fedha Afrika (MIFA) na kufadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). 

Utoaji wa tuzo hiyo hulenga kuutambua mchango wa marais waliofanya vizuri katika ujenzi wa miundombinu barani Afrika na kuuenzi mchango wa aliyekuwa Rais wa benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB 1985-1995) Babaye Ndiaye kutokana na kujitoa katika kukuza sekta ya miundombinu Africa. 

Rais Samia amesema mafanikio katika sekta ya miundombinu yamechangiwa na maraisi wote waliopita hasa kuanzia awamu ya tatu chini ya hayati Benjamin Mkapa, ambapo hayati Magufuli ndiye alitumika zaidi katika ujenzi wa miundombinu akihudumu kama waziri ujenzi na uchukuzi kabla ya kuwa kiongozi wa juu nchini.

“Kama tuzo hii alitakiwa apewe mtu mmoja kuliko Watanzania wote basi mtu huyo ni John Pombe Magufuli ni bahati mbaya hayupo pamoja nasi aweze kushuhudia matunda ya kazi yake,” amesema Samia wakati akitoa salamu za shukrani mara baada ya kutangazwa mshindi wa tuzo hiyo kwa mwaka 2022.

Rais Samia anakuwa rais pekee mwanamke kuchukua tuzo hii barani Afrika tangu ilivyoanzishwa 2016.

error: Content is protected !!