Sekta ya utalii Kenya yakabiliwa na changamoto, watalii wahamia nchi jirani

HomeKitaifa

Sekta ya utalii Kenya yakabiliwa na changamoto, watalii wahamia nchi jirani

Enzi ambazo watalii walipotoshwa kuamini kuwa Mlima Kilimanjaro uko Kenya zimeanza kupotea, huku wengi wao sasa wakihamia vivutio vya utalii katika mataifa mengine ya Afrika Mashariki. Mwelekeo huo unaelezwa kuanza kuathiri uchumi wa Kenya na kudhoofisha sekta ya utalii, hasa kutokana na changamoto za miundombinu duni na huduma zisizoridhisha.

Watalii waliohojiwa jijini Nairobi wiki hii wamelalamikia gharama kubwa za kuingia katika hifadhi za wanyama, hususan Maasai Mara, pamoja na hoteli zilizochakaa na msongamano mkubwa katika maeneo maarufu ya utalii. Baadhi yao wamesema barabara mbovu na hofu ya usalama imepunguza mvuto wa kutembelea Kenya na kuwalazimisha kutafuta huduma bora na maeneo tulivu zaidi katika nchi jirani za Afrika Mashariki.

Uchambuzi unaonyesha kuwa sababu kuu za kushuka kwa sekta ya utalii nchini Kenya ni pamoja na miundombinu duni, gharama kubwa za huduma na changamoto za usalama. Ripoti ya Wizara ya Utalii na Wanyamapori ya Novemba 5, 2025, inaonyesha kiwango cha chini cha ubora wa miundombinu ya usafiri wa anga kilichopata alama 3.21 na miundombinu ya usafiri wa nchi kavu pamoja na bandari kupata alama 3.23, viwango ambavyo viko chini ya wastani wa kimataifa.

Watalii pia wamelalamikia ubora mdogo wa huduma na vifaa vya utalii ukilinganisha na mataifa kama Mauritius na Afrika Kusini. Tathmini nyingine inaonyesha huduma za utalii nchini Kenya zimepata alama ya 1.25, kiwango kinachotajwa kuwa miongoni mwa vya chini zaidi katika maeneo makuu ya utalii barani Afrika.

Mapungufu makubwa yamebainishwa katika alama za maelekezo kwa wageni, huduma za mapokezi, upatikanaji wa maji safi na usimamizi wa taka, hali inayopunguza kuridhika kwa watalii na muda wao wa kukaa nchini humo.

error: Content is protected !!