Serikali imesema imeongeza aina za dawa muhimu za afya ya akili kutoka 21 mwaka 2021 hadi 36 mwaka 2026 ili kuboresha matibabu na upatikanaji wa dawa kwa wananchi wenye changamoto za afya ya akili nchini.
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema hayo leo Oktoba 19, 2026 wakati akiwasilisha taarifa ya Wizara kuhusu hali, athari na mikakati ya kukabiliana na changamoto za afya ya akili nchini mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa.
“Maboresho haya yamejumuishwa katika Mwongozo wa Matibabu na Orodha ya Dawa Muhimu (STG–NEMLIT) ulioanza kutekelezwa mwaka 2026, yakilenga kuongeza chaguo la matibabu kwa kuzingatia mahitaji ya wagonjwa na uwezo wao wa kumudu gharama,” amesema Dkt. Samizi.
Aidha, Dkt. Samizi amesema Serikali pia imeimarisha huduma za afya ya akili katika ngazi ya jamii ambapo wahudumu elfu 9,545 wamepatiwa mafunzo na wengine elfu 1,022 wanaendelea na mafunzo.
“Hadi kufikia Septemba 2026, wananchi zaidi ya elfu 4,000 walikuwa wamepata uchunguzi wa awali wa sonona katika mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma kupitia huduma zinazotolewa na wahudumu wa afya waliofunzwa,” amesema Dkt. Samizi
Katika kukabiliana na upungufu wa wataalamu, Serikali imeimarisha mafunzo katika vyuo vya MUHAS, Mirembe na Chuo Kikuu cha Dodoma ili kuongeza idadi ya wataalamu wa afya ya akili na kusogeza huduma karibu na wananchi.


