Kadogosa amwondoa Meneja wa TANROADS Songwe

HomeKitaifa

Kadogosa amwondoa Meneja wa TANROADS Songwe

Waziri wa Ujenzi, Masanja Kadogosa, amemuondoa katika nafasi yake Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Songwe Mhandisi Fredrick Mande, na kumtaka kurejea makao makuu ya TANROADS, kufuatia kushindwa kusimamia ipasavyo mradi wa ujenzi wa barabara ya Forodha – OSBP – Tunduma yenye urefu wa mita 1,675, mpakani mwa Tanzania na Zambia.

Hatua hiyo imekuja baada ya Waziri Kadogosa kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo usiku wa Oktoba 15, 2026, akitekeleza maelekezo ya Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, ambaye awali alieleza kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo licha ya Serikali kutoa sehemu kubwa ya fedha za mradi.

Mradi huo unaotekelezwa na Serikali kwa lengo la kuboresha mtiririko wa magari na mizigo katika mpaka wa Tanzania na Zambia, kupunguza msongamano wa magari, kuongeza ufanisi wa huduma za forodha na kurahisisha huduma za biashara za kikanda umeoneshwa kusuasua licha ya kutakiwa kukamilika ifikapo Oktoba 31, 2026 kwa mujibu wa kimkataba.

Aidha, Kadogosa amempa mkandarasi wa mradi huo muda wa wiki mbili kukamilisha kazi zilizobaki, huku akiahidi kurejea eneo hilo ndani ya siku saba kukagua utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa na kujiridhisha kuwa kasi ya ujenzi imeongezeka.

Kadhalika, Waziri huyo ametoa maelekezo kwa Mameneja wote wa TANROADS nchini kuhakikisha kila mradi wa ujenzi unasimamiwa kwa uwazi na uwajibikaji, huku akisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa pande tatu zenye majukumu tofauti, ambazo ni msimamizi wa mradi, mkandarasi na msimamizi anayewakilisha Serikali.

 

error: Content is protected !!