Tanzania yaunga mkono mkakati wa Benki ya Dunia wa kukuza ajira kwa vijana

HomeKitaifa

Tanzania yaunga mkono mkakati wa Benki ya Dunia wa kukuza ajira kwa vijana

Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Omar (Mb) amesema Tanzania inaunga mkono mkakati maalum wa Benki ya Dunia wa kuzisaidia nchi wanachama kuweka mipango ya maendeleo na miradi itakayochochea upatikanaji wa ajira hususan kwa vijana na kukuza sekta binafsi ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi.

Balozi Omar amesema hayo jijini Bangkok nchini Thailand, wakati wa Mkutano wa Kundi la Kwanza la nchi za Kanda ya Afrika, wanachama wa Benki ya Dunia, uliofanyika kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, inayoendelea nchini humo.

Amesema ajira ni suala la kipaumbele kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya watu, ambayo sehemu kubwa inaundwa na watoto na vijana wanaohitaji fursa za elimu, ujuzi na ajira ili kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi.

Ameeleza kuwa serikali itaendelea kuwekeza katika elimu na ukuzaji wa ujuzi ili kuwawezesha vijana kupata ajira na kujiajiri, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza fursa za ajira kupitia sekta zenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira nchini zikiwemo Sekta za kilimo, uchimbaji na uchakataji wa madini pamoja na utalii.

Balozi Omar amesema lazima kuongeza juhudi si tu katika uzalishaji wa mazao pekee, bali katika kuongeza thamani kupitia usindikaji na uanzishaji wa viwanda vinavyotumia malighafi za ndani, hatua itakayo ongeza fursa za ajira, kukuza biashara na kuimarisha mchango wa sekta hiyo katika uchumi.

Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa nchini inatoa fursa kwa sekta binafsi, hususan wawekezaji wa ndani, kushiriki katika utekelezaji wake na kunufaika na fursa za kiuchumi zinazotokana na uwepo wa miradi hiyo.

error: Content is protected !!