Sh. bilioni 241 kutekeleza vipaumbele vya Wizara ya Mambo ya Nje

HomeKitaifa

Sh. bilioni 241 kutekeleza vipaumbele vya Wizara ya Mambo ya Nje

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba ametaja vipaumbele vitano vya wizara hiyo katika Mwaka wa Fedha 2024/25.

Akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2024/25 bungeni mjini Dodoma leo, Waziri Makamba ametaja vipaumbele hivyo kuwa ni kuratibu utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi ili kuchochea uwekezaji, utalii, na biashara pamoja na kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa maendeleo ya nchi kwa ujumla.

“Kuendelea kuimarisha uratibu na ushirikiano wa uwili pamoja na ushiriki wa Tanzania katika jumuiya na mashirika ya kikanda na kimataifa ili kulinda maslahi ya taifa; pamoja na kustawisha diplomasia ya kisasa na kujenga uhusiano wa karibu na nchi washirika.

“Kuongeza ushawishi wa Tanzania kwa nchi nyingine katika masuala mtambuka, kwenye Jumuiya na Mashirika ya Kikanda na Kimataifa,” amesema na kutaja vipaumbele vingine ni kushiriki kwenye jitahada za kikanda na kimataifa za kudumisha amani, ulinzi na usalama.

“Kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi, kuimarisha utawala bora na rasilimaliwatu pamoja na kutekeleza miradi ya ujenzi, ununuzi na ukarabati wa majengo ya ofisi, makazi ya watumishi na vitega uchumi katika balozi za Tanzania na makao makuu,” amesema.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeomba bunge liidhinishe jumla ya Sh 241,069,232,000, kati ya fedha hizo Sh 229,435,856,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh 11,633,376,000 ni kwa ajili ya bajeti ya maendeleo.

error: Content is protected !!