Dkt. Kikwete kinara utafutaji fedha za kuimarisha elimu Afrika

HomeKitaifa

Dkt. Kikwete kinara utafutaji fedha za kuimarisha elimu Afrika

Rais Mstaafu Dk Jakaya Kikwete kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Ubia wa Elimu Duniani (GPE) ameshiriki Mkutano wa Mwaka 2024 wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB 2024 Annual Meeting) unaofanyika jijini Nairobi, Kenya Mei 26 – 28, 2024.

Ametumia fursa ya kushiriki mkutano huo kuzungumza na vongozi mbalimbali, hususan kutoka sekta za kifedha, sekta binafsi na washirika wa kimaendeleo kuhusu umuhimu wa kuongeza ufadhili wa kifedha ili kuimarisha mpango wa utoaji chakula kwa wanafunzi wakiwa mashuleni pamoja na kuhamasisha ubunifu wa mbinu mpya za kufadhili elimu ya juu, elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.

Taasisi ya GPE ambayo Rais Mstaafu Kikwete ni Mwenyekiti wa Bodi imejikita katika kujenga ubia na wadau mbalimbali wa kimataifa na ndiyo Taasisi kinara duniani inayohamasisha jitihada za kuzisaidia nchi zaidi ya 76 kuimarisha mifumo yao ya elimu ili kutoa elimu bora zaidi kwa watoto wa kike na wa kiume, hususan wale wanaotoka katika mazingira duni, wenye ulemavu na wanaoathiriwa na majanga kama vile vita na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wa Afrika, GPE ina miradi inayozunufaisha nchi 40, ikiwemo Tanzania. Tangu mwaka 2016 hadi sasa, Taasisi ya GPE imetoa msaada wa zaidi ya Sh bilioni 250 za Kitanzania kufadhili programu hiyo ya utoaji wa chakula mashuleni katika nchi inapofanya shuhuli zake.

Katika Mkutano huo, pamoja na mambo mengine, Rais Mstaafu Kikwete alieleza umuhimu wa washiriki kufikiria mbinu mpya za kupata fedha zitakazotumika kugharamia programu za kutoa chakula mashuleni kwani ukweli ni kwamba licha ya jitihada kubwa inayofanyika na nchi nyingi za kipato cha chini na kati katika kuimarisha programu hiyo, bado zinakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kuelemewa na madeni.

error: Content is protected !!