Siku nne Katavi: Rais Samia aridhishwa na maendeleo

HomeKitaifa

Siku nne Katavi: Rais Samia aridhishwa na maendeleo

Rais Samia Suluhu Hassan amemaliza ziara yake ya siku nne mkoani Katavi akieleza kuridhishwa na maendeleo yaliyopatikana na matumizi bora ya fedha kutoka Serikali Kuu katika kutatua kero za wananchi. Katika hotuba yake, Rais Samia alitoa pongezi kwa wakulima wa mkoa huo kwa juhudi zao za kuzalisha chakula na kusema kuwa Katavi ina nafasi kubwa katika kuilisha Tanzania ikishirikiana na mikoa mingine kama Rukwa.

Akizungumza katika eneo la Kibaoni, Rais Samia alisema, “Katavi ni wazalishaji wazuri wa chakula, nataka niwaahidi kwamba serikali imeendelea kuongeza fedha katika sekta ya kilimo na kwa mkoa huu tunajitahidi kufanya kila linalowezekana ili uzalishaji uongezeke.”

Rais alibainisha kuwa serikali imewekeza katika ujenzi wa skimu za umwagiliaji 29 na ina mpango wa kuongeza nyingine sita. Pia, maghala ya kuhifadhia chakula yamejengwa na serikali inaendelea na jitihada za kujenga zaidi ili Katavi iweze kujitegemea katika uzalishaji na uhifadhi wa chakula. “Tunajitahidi kuleta huduma za ugani na kujenga mabwawa ili tutakapofikwa na kiangazi mabwawa yawe yana maji na watu waendelee na kilimo,” aliongeza Rais Samia.

Mtoto aliyejitokeza kumsikiliza Rais Samia Suluhu alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kibaoni wakati akimaliza ziara yake mkoani Katavi

Rais pia alisifu ukarimu wa watu wa Katavi na ushirikiano wao katika kila hatua ya ziara yake, akisema, “Naushukuru sana mkoa wa Katavi kwa ziara nzuri, ziara iliyonionyesha maendeleo, ziara iliyonionyesha ukarimu wa watu wa Katavi kwakweli watu wa Katavi ni wakarimu. Ziara iliyonionyesha ushirikiano na upendo kwa sababu kila ninapokwenda watu ni wengi wanatokeza kuja kunilaki na kuja tuzungumze, niwasikie na wanisikie.”

Ziara ya Rais Samia mkoani Katavi imeacha ujumbe wa matumaini na ahadi za maendeleo zaidi katika sekta ya kilimo na huduma za kijamii, huku ikionyesha jinsi mkoa huo unavyoendelea kuwa tegemeo katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara nchini Tanzania.

 

 

error: Content is protected !!