Suala la wabunge 19 tuiachie mahakama

HomeKitaifa

Suala la wabunge 19 tuiachie mahakama

Rais Samia Suluhu Hassan amesema hawezi kuingilia kati suala la Wabunge 19 wanaodaiwa kuwa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kutaka mahakama iachwe ifanye kazi yake.

Rais Samia aliyekuwa akihutubia kongamano la Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) jana Machi 8, 2023 mkoani Kilimanjaro ametoa kauli hiyo alipokuwa akijibu maombi ya Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe la kutaka wabunge hao waondolewe Bungeni kwa sababu chama hicho hakikuwateua na tayari kilishawavua uanachama.

“Naomba niwaambie tuache mkondo ule uendelee, tutizame mbele yanayokuja, si rahisi mimi kama Rais kutia mkono huko,” amesema Rais Samia.

Kauli ya Rais Samia kuhusiana na jambo hilo ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu na maelfu ya wafuasi na wanachama wa Chadema ambao mara kadhaa walikuwa wakimkumbushia katikati ya hotuba yake ambapo baadhi walisikika wakisema “Covid-19”.

Kabla ya Mbowe kutoa ombi hilo, Mwenyekiti wa Bawacha Taifa Sharifa Suleiman naye alimuomba Rais kulitazama jambo hilo kwa jicho la tatu.

“Natambua kuwa si vema kuzungumzia kesi ambayo ipo mahakamani, lakini kwa niaba ya Bavicha nakuomba ulitizame hili kwa jicho la tatu, “ amesema Sharifa.

Itakumbukwa wabunge 19 wanaolalamikiwa akiwemo Halima Mdee na Esther Matiko, wanadaiwa kughushi nyaraka zilizowatambulisha kama wabunge wa viti maalumu kutoka Chadema ambapo chama hicho kilikana kuhusika na kuwavua uanachama Mei 11, 2022.

Julai 24, mwaka 2022 wabunge hao walifungua shauri mahakamani kupinga kuvuliwa uanachama wakisema hawakuridhishwa na mchakato kwani walipokea vitisho na hawakupewa nafasi ya kusikilizwa.

Pamoja na jambo hilo kuzua mijadala mbalimbali Spika wa Bunge la Tanzania Dk Tulia Akson mara kadhaa amesikika akisema uhalali au ubatili wa wabunge hao kuwepo bungeni utabainika pale tu mahakama itakapotoa maamuzi yake.

Kesi hiyo ya Wabunge hao inatarajiwa kuendelea Machi 9 na 10 ambapo baadhi ya viongozi wa Chadema wataitwa kutoa ushahidi wao.

error: Content is protected !!