Jumla ya Taasisi za ndani 76 na nje 12 zimepata kibali cha kuwa waangalizi wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Jaji Mstaafu Jacobs Mwambegele ametoa taarifa hiyo wakati akifungua kikao kazi kati ya tume hiyo na viongozi wa vyama vya siasa nchini mkoani Dodoma jana Julai 27, 2025.
Jaji Mwambegele amesema waangalizi hao wamepatikana baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa na tume hiyo.
“Tume tayari imetoa kibali cha elimu ya mpiga kura kwa taasisi na asasi 164. Vilevile tume ilitoa mwaliko kwa taasisi na asasi za ndani ya nchi zenye nia ya kuwa waangalizi wa uchaguzi kuleta maombi. Baada ya mchakato wa uhakiki jumla ya taasisi na asasi 76 za ndani na 12 za kimataifa zimepata kibali.” Amesema jaji Mwambegele.
Aidha, Jaji Mwambegele ametoa rai kwa vyama vya siasa na wafuasi wake kufanya kampeni za kistaarabu ili kuepika kufanya vitendo vitakavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu wa nchi kutokana na joto kali la kisiasa linalosababishwa na kampeni za uchaguzi.