Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetahahdarisha umma kuwepo vipindi vya upepo mkali katika Bahari ya Hindi kwa siku tatu mfululizo kuanzia leo.
TMA kupitia taarifa yake iliyotoka jana kwa umma, ilisema upepo huo unatarajiwa kuwa na kasi ya kilomita 40 kwa saa na kusababisha mawimbi makubwa yanayofikia urefu wa mita mbili.
Ilitja maeneo yatakayoathiriwa na hali hiyo ni baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani ya bahari ya Hindi ikibainisha mikoa ya Lindi na Mtwara. Maeneo mengine ni Tanga na Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia, Dar es Salaam ikiwemo Unguja na Pemba.
Kwa mujibu wa TMA, matokeo ya Utabiri wake yataathiri baadhi ya shughuli za uvuvi na usafirishaji baharini na kupeperushwa kwa vumbi katika baadhi ya maeneo hususan yaliyoko karibu na pwani ya bahari.