Tamko kuhusu IST kupita daraja la Tanzanite

HomeKitaifa

Tamko kuhusu IST kupita daraja la Tanzanite

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam , ACP Jumanne Muliro ametoa ufafanuzi kuhusu taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinazosema  Jeshi la Polisi limepiga marufuku gari aina ya IST na PASO kupita daraja la Tanzanite kwamba ni za uongo hivyo wananchi wapuuze tangazo hilo.

“Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar Es Salaam linautaka Umma uelewe kuwa halijawahi kutoa taarifa hiyo inayosambaa kwenye vyombo mbali mbali vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii hivyo taarifa hizo sio za kweli na Jeshi halijajua malengo yake ni nini.” alisema Muliro.

Taarifa hiyo imeambatanishwa na picha za Kamanda Muliro na kuonyesha iliripotiwa na chombo cha habari cha Millard Ayo, lakini pia kilikanusha nakusema hawahusiki na kusambaza ujumbe huo.

“Jeshi linafanya uchunguzi kujua aliyezitoa kwani hata Millard Ayo amekanusha kuwa ukurasa uliotumika si wake.” alisema Muliro.

Aidha, Kamanda Muliro ameutaka umma kupuuza taarifa hizo na kusema kwamba sheria itachukua mkondo wake kwa mtu au kikundi kitakachojihusisha na upotoshaji wa taarifa.

“Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar Es Salaam limeelekeza kuwa halitavumilia kuwepo kwa Mtu/kikundi ambacho kimejikita katika kupotosha taarifa mbali mbali kwa umma , misingi ya kisheria itafuatwa ili kuwabaini na kuwafikisha kwenye mamlaka za kisheria watu wanaofanya vitendo hivyo.” alisema Muliro.

error: Content is protected !!