Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde wakati wa kikao na mazungumzo na Ujumbe maalum wa wataalamu sita wa madini kutoka Korea Kusini ukiongozwa na Mtaalam kutoka Taasisi ya Jiosayansi na Rasilimali Madini ya Korea (KIGAM), Seong-Jun Cho.
“Huu ni utekelezaji wa Dira ya Madini 2030, Serikali imewezesha kuanzishwa kwa mradi wa ujenzi wa kituo cha kisasa na kikubwa cha Teknolojia ya madini mkakati pamoja na ununuzi wa vifaa vya kisasa vya utafiti wa kina wa madini na Dkt. Samia ametuelekeza kuongeza eneo la utafiti kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030”. Amesema Mavunde
Mradi huo ambao unatarajia kugharimu Woni za Korea Bilioni 21.8 (sawa na Dola za Kimarekani Milioni 16.5) utahusisha kuanzishwa kwa Kituo cha Teknolojia ya Madini; Uchunguzi wa pamoja wa Mfumo wa Kidijitali wa Taarifa za Rasilimali Madini; Ujenzi wa uwezo wa wataalamu na Utekelezaji wa mifumo ya ESG ya madini.
“Utekelezaji wa mradi huu ni matokeo ya makubaliano ya mashirikiano baina ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Taasisi ya KIGAM ya Korea Kusini kupitia MoU iliyosainiwa tangu Mwaka 2024 na mradi huu unaonesha wazi dhamira na azma ya Serikali yetu katika kufikia malengo tuliyojiwekea”. Ameongeza Mavunde
Utekelezaji wa mradi huo wa miaka mitano unatarajiwa kukamilika mwaka 2031 huku ukiangazia kwa kina madini ya nikeli sambamba na kutoa nafasi kwa wachimbaji wadogo kupata mafunzo maalum yatayoongeza ufanisi na tija ya shughuli zao huku serikali ikiwaomba KIGAM kuangalia uwezekano wa kusaidia kujenga uwezo zaidi ili mradi huo uweze kufanikiwa ipasavyo.


