Tanzania kupata bil 49/- kukabili athari mabadiliko tabianchi

HomeKitaifa

Tanzania kupata bil 49/- kukabili athari mabadiliko tabianchi

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotarajia kunufaika na Dola za Marekani milioni 20 (sawa na Sh bilioni 48.9) kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kupitia Mfuko wa Kukabiliana na Hasara na Uharibifu.

Hayo yalisemwa na Mshauri wa Rais katika masuala ya mazingira na Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (AGN), Dk Richard Muyungi alipokutana na Watanzania wanaoshiriki Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa wa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP 30) unaoendelea katika Jiji la Belem nchini Brazil.

Dk Muyungi alisema katika utekelezaji huo, tayari zimetengwa Dola za Marekani milioni 250 kwa mwaka ujao, kwa ajili ya kufadhili miradi hiyo ambayo Tanzania ni nchi mnufaika. “Nasisitiza huu sio mkopo, bali ni ufadhili na hadi sasa tuna mambo ya kufuatilia na sisi kama nchi tumepewa kipaumbele.

Hivyo, tunaweza kuwa na miradi hata miwili ambayo inaweza kuwa na manufaa makubwa. Naomba Ofisi ya Makamu wa Rais tuteue mtu mmoja, yaani ‘focal person’ (mhusika mkuu) kwa ajili ya Mfuko wa Kukabiliana na Hasara na Uharibifu,” alisema.

Alibainisha kuwa, mwaka 2025 Tanzania imeteuliwa kuwa Kituo cha Santiago ambacho kitakuwa kinaratibu msaada wa kiufundi kwa nchi zinazoathiriwa na hasara na uharibifu unaotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, Dk Muyungi aliomba Watanzania kutoka serikalini na sekta binafsi wanaoshiriki mkutano huo wenye takribani washiriki 60,000 kusimama kama nchi na kujenga mitandao ya kuchangamkia fursa ili kuendelea kuinufaisha nchi.

“Kama tunavyoona hapa COP 30 yapo mabanda mengi yenye wingi wa washiriki. Nawaomba tutumie fursa hii kutengeneza mtandao. Tuna timu ya majadiliano, tufuatilie fursa za benki, NGOs (Mashirika Yasiyo ya Kiserikali) na serikali ili tukitoka hapa, tutoke na faida,” alisisitiza.

Vilevile, Dk Muyungi alitumia nafasi hiyo kuwaeleza washiriki hao kuwa wana jukumu la kuitangaza Dira ya Maendeleo 2025 na Serikali ya Tanzania imetekeleza mambo gani ya msingi kwa wananchi, hivyo kuchagiza upatikanaji wa fursa zaidi kwa maendeleo endelevu.

error: Content is protected !!